Marais Donald Trump na Abdel Fattah el-Sisi waijadili Iran
Ikulu ya Marekani imetangaza kwamba Rais Donald Trump wa nchi hiyo asubuhi ya leo amefanya mazungumzo ya simu na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri kuihusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo ya marais hao yalijikita juu ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia kwa serikali halali ya Syria katika vita vyao dhidi ya ugaidi na kuutaja uungaji mkono huo kuwa usio wa kimajukumu. Kadhalika Trump na El-Sisi wamesisitiza umuhimu wa kuimarishwa mahusiano baina yao kwa ajili ya kile walichokisema eti ni kupatikana umoja kati ya nchi za Kiarabu na kudumishwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati. Katika miezi ya hivi karibuni Marekani na washirika wake wamekuwa wakifanya njama chungu nzima kwa ajili ya kuzuia kushindwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji nchini Syria na Iraq, ingawa njama zao hizo hazijafanikiwa.
Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya makundi mbalimbali ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudia, Marekani na waitifaki wao katika eneo kuanzisha mashambulizi makali nchini humo kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Damascus ili kuudhaminia usalama utawala haramu wa Israel. Kufuatia hali hiyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kushirikiana na Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na Russia ziliingilia kati katika kupambana na makundi ya kigaidi, hususan lile la Daesh (ISIS) suala ambalo halikuifurahisha Washington, Riyadh na washirika wao.