Mar 28, 2018 02:33 UTC
  • Kukiri Saudi Arabia nafasi ya Marekani katika kuenea Uwahabi

Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia amekiri katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Washington Post kwamba, nchi yake imejikita zaidi katika kueneza Uwahabi ulimwenguni kwa takwa la Marekani na kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya Mashariki katika kipindi cha Vita Laini vya 1947-1991.

Bin Salman amekiri pia kuwa, utawala wa Saudi Arabia umekuwa ukiudhamini kwa fedha Uwahabi na kwamba, kikawaida hilo hutimia kupitia asasi za Saudia zinazofanya shughuli zake katika sekta binafsi ndani ya nchi hiyo. Chimbuko la kifikra la akthari ya magenge ya kigaidi na kitakfiri yenye mielekeo ya kufurutu ada na upotofu katika dini ni Uwahabi.

Itikadi hizi potofu zimekuwa na nafasi muhimu katika kuibuka harakati za kigaidi na za uingiliaji mambo ya nchi nyingine sambamba na hatua za ufitinishaji za Aaal Saud katika Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla. Kuleta anga ya hofu na kueneza mapigano ya kikaumu na kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu ndio msukumo mkuu wa wazushaji fitina wa Kiwahabi wa kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri lengo hasa likiwa ni kuleta mpasuko na migawanyiko miongoni mwa nchi za Kiislamu.

Uwahabi

Mawahabi wenye kuchupa mipaka mbali na kufanya njama za kuzusha vita vya ndani kwa kutumia fimbo ya utakfiri, wamesimama kwa ajili ya kuanzisha vita dhidi ya madhehebu na makundi yote ya Kiislamu na ghairi ya fikra na mitazamo yao tu, wanazitambua fikra za wengine kwamba, ni batili za kikafiri. Kimsingi ni kuwa, Mawahabi hawana mpaka na ndio maana matokeo mabaya ya itikadi zao hizo potofu yamewakumba hata waanzilishi, waungaji mkono na waenezaji wake.

Nafasi ya Saudi Arabia katika kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri, kuenea kwake pamoja na kuyaongoza kifikra makundi hayo potofu na yenye kutenda jinai ni ukweli ambao kwa hakika umekiriwa na duru za magazeti na vyuo vikuu vya Magharibi. Gazeti la Telegraph la nchini Uingereza sambamba na kuutaja Uwahabi kama chimbuko kuu la ugaidi wa kimataifa linaeleza sababu zake. Gazeti hilo linaandika kuwa, chimbuko la kundi la kigaidi la Daesh linarejea katika Uwahabi ambao kimsingi una fikra za kuchupa mipaka na makao makuu yake ni Saudi Arabia.

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia

Makundi ya Daesh, Jabhat al-Nusra, al-Qaeda na Taliban yametokana na fikra na Kiuwahabi za Saudi Arabia na kila mojawapo kati ya makundi hayo limejifunza utakfiri katika shule za Saudia na kusukuma mbele gurudumu la mipango yake.  Ukweli ni kuwa, Uwahabi ni chimbuko la kulea na kueneza ugaidi. Saudia ikiwa muenezaji wa fikra za Kiwahabi na Kisalafi imekuwa chanzo na kitovu cha kulea ugaidi na kuupeleka katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Kuwa pamoja viongozi wa Marekani hasa Rais Donald Trum wa Marekani na Uwahabi wa Saudi Arabia ndiko kunakoelezwa na wajuzi wa mambo kuwa, chanzo kikuu cha ugaidi na kuenea kwake ulimwenguni na hivyo kuifanya dunia ikabiliwe na hatari kubwa.

Profesa Paul Atwood, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Massachusetts nchini Marekani anaamini kwamba, Saudi Arabia na Marekani ndio chimbuko la kuenea misimamo mikali na kukua kundi la kigaidi la Daesh katika Mashariki ya Kati. Anasema: Ugaidi ni wenzo unaotumiwa na Marekani kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za kigeni.

Wapiganaji wa kundi la Daesh lenye fikra za Kiwahabi

Gazeti la Huffington Post nalo limekiri kwamba, Saudi Arabia na Uwahabi ndio waungaji mkono halisi wa ugaidi ulimwenguni. Kiujumla ni kuwa, utawala wa kifalme wa Aal Saud unaotawala nchini Saudi Arabia ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa kabisa na waleaji wa fikra za kigaidi ulimwenguni.

Hii ni katika hali ambayo, Marekani nayo kutokana na kushirikiana na utawala wa Riyadh na katika fremu ya siasa zake za kutanguliza mbele maslahi yake sambamba na kunufaika zaidi na harakati za makundi ya kigaidi ili kutekeleza mipango yake ya kuzusha fitina, imeliweka katika ajenda zake suala la kuendelea kusimamia na kueneza makundi yenye misimamo ya kigaidi.

Ushahidi wote unaonyesha kuwa, kushadidi mauaji, utumiaji mabavu, misimamo ya kuchupa mipaka na ukosefu wa amani na usalama duniani, ni matokeo ya siasa za Saudia za kueneza fikra za Kiwahabi kwa uungaji mkono wa Marekani.

Tags