Vikosi vya usalama Bahrain vyawashambulia waandamanaji
Maafisa usalama wa Bahrain wamewashambulia wananchi waliokuwa wamemininika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kufanyika nchini humo mashindano ya magari ya Langalanga maarufu kama Formula 1.
Katika maandamano hayo yaliyofanyika jana Ijumaa katika mji wa Bilad al-Qadeem, waandamanaji kadhaa walijeruhiwa na wengine wengi kutiwa mbaroni.
Wanaharakati wa haki za binadamu walioshiriki maandamano hayo wanasema ni kichekesho jamii ya kimataifa kuruhusu mashindano hayo ya kimataifa ya Grand Prix, a Formula One kufanyika katika hali ambayo utawala wa Aal-Khalifa unaendelea kuwakandamiza wananchi.
Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International tawi la Bahrain imewataka mashabiki wa mashindano hayo ya magari ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo tangu mwaka 2004 kuishinikiza serikali ya Manama kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa.
Utawala wa kiimla wa Bahrain uliwakamata wapinzani zaidi ya 50 mwezi uliopita pekee huku ukandamizaji ukiendelea kushika kasi nchini humo.
Tarehe 14 Februari mwaka 2011 wananchi wa Bahrain walianzisha vuguvugu la mapambano kwa kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa.