Rais Assad arejesha nishani aliyopewa na 'Mtumwa wa Marekani'
(last modified Fri, 20 Apr 2018 07:24:09 GMT )
Apr 20, 2018 07:24 UTC
  • Rais Assad arejesha nishani aliyopewa na 'Mtumwa wa Marekani'

Rais Bashar al Assad wa Syria amerejesha nishani bora zaidi ya Ufaransa aliyotunukiwa na Rais Jacques Chirac mwaka 2001 na kusema hawezi kubakia na zawadi ya nchi ambayo ni mtumwa wa Marekani na ambayo imedondosha mabomu Syria.

Ofisi ya Rais wa Syria imetangaza kuwa, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imerejesha nishani ya Légion d'honneur aliyotunukiwa Rais Assad. Taarifa hiyo imesema nishani hiyo imekabidhiwa Ubalozi wa Romania mjini Damascus ambao unawakilisha maslahi ya Ufaransa.

Taarifa hiyo imesema, uamuzi wa kurejesha nishani hiyo ya juu kabisa umetokana na kushiriki Ufaransa katika hujuma iliyoshirikisha Uingereza na Marekani mnamo Aprili 14 dhidi ya Syria. Aidha taarifa hiyo imesema, "Rais Assad ameona ni jambo lisilofaa kuendelea kubakia na nishani aliyotunukiwa na 'nchi ambayo ni mtumwa wa Marekani' na ambayo inaunga mkono magaidi na kukiuka nukta za msingi za sheria za kimataifa.

Nishani ya  Légion d'honneur

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametuhumiwa pia na vyama vya upinzani nchini humo kwa kuvuruga sera huru za kujitegemea za nchi hiyo ambayo ni maarufu kwa kutoshiriki katika hujuma ya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003. Mkuu wa chama cha upinzani cha National Front Marine Le Pen amesema kushiriki Ufaransa katika hujuma dhidi ya Syria kunahatarisha nchi hiyo. Amemkosoa Rais Macron kwa kutokuwa na msimamo huru.