Maelfu ya Waisraeli waandamana kupinga udikteta wa Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43500-maelfu_ya_waisraeli_waandamana_kupinga_udikteta_wa_netanyahu
Maelfu ya Waisraeli wamemiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kile waliochokitaja kama udikteta wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu sambamba na kushinikiza afungwe jela kutokana na kashfa za ufisadi wa kifedha zinazomuandama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2018 09:13 UTC
  • Maelfu ya Waisraeli waandamana kupinga udikteta wa Netanyahu

Maelfu ya Waisraeli wamemiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kile waliochokitaja kama udikteta wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu sambamba na kushinikiza afungwe jela kutokana na kashfa za ufisadi wa kifedha zinazomuandama.

Maandamano hayo yamefanyika mjini Tel Aviv, kukosoa muswada wa sheria ambao iwapo utapasishwa na Bunge la Knesset, basi Mahakama Kuu ya Israel itavuliwa majukumu na uwezo na kisha kutwaliwa na Netanyahu.

Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe zisemazo, "Acha kunyakua mamlaka Bibi (Netanyahu)", "Bibi ondoa mikono yako kwenye Mahakama ya Juu", na "Fisadi, hauna jukumu lolote". 

Muswada huo ambao utaanza kujadiliwa Aprili 29, umekosolewa vikali na watu wa matabaka mbalimbali huko Israel, wanaosema kuwa iwapo utapasishwa basi sheria hiyo itakuwa kinyume cha katiba.

 

Maandamano dhidi ya Netanyahu mjini Tel Aviv

Maandamano ya kutaka kumuondoa madarakani Netanyahu na kuharakishwa uchunguzi dhidi yake yalianza miezi kadhaa iliyopita mjini Tel Aviv na katika maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi na kupokea rushwa ya mamilioni ya dola kutoka kampuni moja ya Ujerumani zinazomkabili Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ulianza tangu Januari Pili mwaka jana 2017.