Je, Israel inatumia 'risasi za sumu' dhidi ya Wapalestina Gaza?
Madaktari wa Palestina na wa kimataifa wameonyesha wasi wasi mkubwa walionao kuhusiana na majeraha mabaya yaliyosababishwa na risasi za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina katika mpaka wa Gaza.
Madaktari katika Hospitali ya Shifa iliyoko Gaza wamesema katika miaka ya hivi karibuni na hususan tangu Israel iivamie Gaza mwaka 2014, hawajawahi kuona majeraha mabaya ya risasi za utawala haramu wa Israel kwa Wapalestina kama sasa.
Kadhalika Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema timu yao imewatibu mamia ya Wapalestina waliokuwa na majeraha ambayo sio ya kawaida ya risasi, na kwamba aghalabu yao wamesababishiwa ulemavu wa maisha kutokana na ukali wa risasi hizo.
Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kufikia sasa katika maandamano hayo ya amani imepindukia 37, huku maelfu ya wengine wakiachwa na majeraha mabaya ya risasi.
Maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' yaliyoitishwa na Wapalestina kwa ajili ya kupigania haki ya kurejea wakimbizi wa taifa hilo katika ardhi zao walizoporwa na Wazayuni mwaka 1948 yalianza Machi 30, na yanatazamiwa kuendelea hadi Mei 15.
Nchi mbalimbali duniani zimeendelea kulaani jinai hizo za Israel na kutaka kuundwa kamisheni huru ya kuchunguza jinai za kutisha zinazofanywa na wanajeshi katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.