Naeem Qassim: Hizbullah haitaweka chini silaha ila baada ya kuangamizwa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43762-naeem_qassim_hizbullah_haitaweka_chini_silaha_ila_baada_ya_kuangamizwa_israel
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, harakati hiyo itakuwa tayari kuweka chini silaha pale tu itakapohakikisha utawala wa Kizayuni wa Israel umeangamizwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2018 11:43 UTC
  • Naeem Qassim: Hizbullah haitaweka chini silaha ila baada ya kuangamizwa Israel

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, harakati hiyo itakuwa tayari kuweka chini silaha pale tu itakapohakikisha utawala wa Kizayuni wa Israel umeangamizwa.

Sheikh Naeem Qassim ameyasema hayo leo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kubainisha kuwa ikiwa Israel inataka kuanzisha mapigano maalumu kwa lengo la kudhoofisha nguvu za Hizbullah na Iran nchini Syria ijue kwamba Iran na Hizbullah ziko macho na zitaizuia isiweze kutekeleza mipango yake hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema, kutokana na kuwepo pande nyinginezo ikiwemo Russia na Iran, vita vyovyote vile vitakavyotokea nchini Syria vinaweza kugeuka kuwa vita vya dunia; kwa hivyo sera za Marekani ni za kupoteza muda na kutoshiriki kwenye mchakato wa kisiasa kabla ya kutokea mabadiliko katika mlingano wa medani za vita, na hilo lenyewe linadhihirisha wasiwasi na hali ya kutapatapa iliyonayo Washington ya kutojua ifuate sera na siasa gani.

Wanajeshi wa Israel wakiwaomboleza askari wenzao walioangamizwa na wapiganaji wa Hizbullah

Katika mahojiano hayo, Sheikh Naeem Qassim, ambaye ni mkuu wa kamati kuu ya kampeni za uchaguzi ya Hizbullah amezungumzia pia uchaguzi wa bunge la Lebanon na kueleza kwamba uchaguzi wa mara hii unatafautiana na chaguzi zilizopita kutokana na kutumika kigezo cha "mlingano" ambacho ni tofauti na kile cha "wingi", hata hivyo Hizbullah ina matumaini ya kupata matokeo mazuri zaidi kuliko iliyopata katika chaguzi zilizopita kwa sababu inaungwa mkono na wananchi pamoja na waitifaki wake.

Uchaguzi wa bunge la Lebanon unatazamiwa kufanyika tarehe 6 ya mwezi ujao wa Mei; na kwa mara ya kwanza utafanyika kwa kutumia kanuni ya "mlingano".

Kwa mujibu wa kanuni ya "mlingano", Lebanon yote itahesabika kama eneo moja la upigaji kura, na kila jamii, kulingana na idadi ya watu wake itakuwa na mwakilishi katika bunge la nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo kanuni iliyopita ya uchaguzi ilikuwa haijumuishi jamii zote za Lebanon, ambapo jamii ndogo ndogo za walio wachache hazikupata fursa ya kushirikishwa katika maamuzi ya kisiasa na hazikuweza kuwa na wawakilishi wao bungeni.../