Malengo mawili ya makelele mapya ya Netanyahu dhidi ya Iran
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Jumatatu usiku aliendeleza vitendo vyake vya chuki na ghilba za kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuonesha mbele ya kamera za vyombo vya habari vitu alivyodai kuwa eti ni ushahidi kwamba Iran inafanya juhudi za siri za kumiliki silaha za nyuklia.
Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Benjamin Netanyahu kufanya propaganda kama hizo za kitoto dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ushahidi uliotolewa na waziri mkuu huyo wa utawala pandikizi wa Israel umekanushwa hata na vyombo vya habari mbalimbali duniani, kiasi kwamba hata gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limeandika, ushahidi uliotolewa na Benjamin Netanyahu kuhusu kufanya Iran harakati za siri za kumiliki silaha za nyuklia ni madai ya zamani sana ambayo yalikuwepo tangu mwaka 1999 hadi 2003.
Amma swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba, lengo la Netanyahu la kutoa madai hayo ya uongo na yaliyopitwa na wakati, ni lipi? Ijapokuwa ulaghai huo wa Netanyahu ni muendelezo wa siasa za kueneza chuki dhidi ya Iran ambazo amekuwa akizifanya kila siku, lakini hivi sasa kuna shabaha mbili kuu zinazofuatiliwa na waziri mkuu huyo wa Israel kabla ya jambo jingine lolote.
Shabaha ya kwanza inahusiana na kipindi hiki cha kutolewa ghilba hizo za waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni. Ulaghai wake huu mpya amezuka nao zikiwa zimebakia siku 12 tu hadi kumalizika muhula wa mwisho wa rais wa Marekani, Donald Trump, wa kutangaza msimamo wake kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kwa kifupi cha JCPOA. Itakumbukwa kuwa, mwezi Januari 2018, Trump alijipa muda wa siku 120 wa kutangaza msimamo wake kuhusu mapatano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumani, na alitishia kuwa msimamo wake utakuwa ni kujitoa katika mapatano hayo. Muhula huo aliojiwekea Trump unamalizika tarehe 12 mwezi huu wa Mei. Hivyo Netanyahu ameamua kuzuka na ghilba hizo mpya ili kujaribu kuhalalisha nia ya Trump ya kujitoa kwenye mapatano hayo.
Hata hivyo, Sayyid Hossein Mousavian, mjumbe wa zamani wa timu ya mazungumzo ya nyuklia na mtafiti katika chuo kikuu cha Princeton huko New Jersey Marekani ameandika makala iliyochapishwa na shirika la habari la Reuters na ndani yake amesema, tangu mwaka 1992, viongozi wa Israel wamekuwa wakifanya kila njia kujaribu kuwakinaisha walimwengu kuwa Iran inataka kumiliki bomu la atomiki ili kwa njia waweze kujipunguzia mashinikizo yaliyowaelemea kutokana na utawala wa Kizayuni wa Israel kumiliki mamia ya mabomu ya nyuklia. Hivyo ulaghai wa mara hii wa kiongozi huyo wa Israel umepangiliwa kwa ujanja wa hali ya juu na shabaha yake kuu ni kuathiri uamuzi wa Trump kuhusu kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Amma shabaha ya pili ya ghilba hizo za Netanyahu inahusiana na hali yake yeye mwenyewe ndani ya utawala wa Kizayuni. Hivi sasa waziri mkuu huyo wa Israel amelemewa na kesi tatu za ufisadi, ukiwemo ufisadi wa fedha, kupokea rushwa na kutumia vibaya madaraka, ambapo ufisadi huu wa kutumia vibaya madaraka unaihusu pia familia yake. Ufisadi huo mkubwa wa Netanyahu umeibua malalamiko makubwa ya wananchi na ukosoaji wa vyama vya kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni. Katika kipindi cha chini ya miezi miwili, Netanyahu atalazimika kwenda kujibu maswali ya polisi wa Israel kuhusu ufisadi wake, hivyo amezuka na madai mapya ya uongo dhidi ya Iran ili kujipunguzia mzigo wa mashinikizo yaliyomuelemea.
Friedman, balozi wa zamani wa Marekani nchini Saudi Arabia anasema, lengo la Benjamin Netanyahu la kutoa tuhuma mpya dhidi ya shughuli za nyuklia za Iran ni kujaribu kupotosha fikra za walio wengi na kuathiri uchunguzi wa polisi ya Israel kuhusu kesi za ufisadi zinazomkabili.