Misri: Inawezekana kutuma nchini Syria vikosi vya Kiarabu
Misri imesema kuwa mazungumzo yanaendelea kufanyika baina ya maafisa wa nchi kadhaa kujadili pendekezo la Marekani la kuunda jeshi la Kiarabu litakalochukua nafasi ya wanajeshi wa Marekani waliopo Syria.
Sameh Shoukr Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa ni jambo linalowezekana kutuma wanajeshi huko Syria watakaochukua nafasi ya vikosi vya Marekani ambao watakuwa Waarabu. Shoukry amenukuliwa na gazeti la al Ahram akisema kuwa pendekezo lililotolewa na Marekani si tu kuwa linajadiliwa na duru za habari bali pia linajadiliwa na maafisa wa nchi kadhaa za Kiarabu kuangalia namna mawazo hayo yanavyoweza kuchangia kurejesha utulivu huko Syria.
Itakumbukwa kuwa, ripoti zilifichua mwezi uliopita kwa kuwanukuu maafisa wa Marekani kuwa utawala wa Rais Donald Trump unataka kuasisiwa muungano wa jeshi la Kiarabu litakalochukua nafasi ya vikosi vya Marekani vilivyopo Syria. Ripoti hiyo iliongeza kuwa serikali ya Washington imewatolea mwito pia nchi waitifaki wake katika eneo hili zikiwemo Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu kuendelea kugharamia vita huko Syria ili kuzuia ushawishi wa Iran baada ya kusambaratishwa kundi la kigaidi la Daesh katika nchi hiyo ya Kiarabu.