Mazungumzo ya kuunda serikali mpya yanaendelea nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i44880-mazungumzo_ya_kuunda_serikali_mpya_yanaendelea_nchini_iraq
Rais Fuad Masum wa Iraq na ujumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Kurdisan leo wameitisha kikao cha kujadili uchaguzi wa hivi karibuni wa nchi hiyo na njia za kushirikiana makundi ya Kikurdi na mirengo mingine bungeni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2018 10:01 UTC
  • Mazungumzo ya kuunda serikali mpya yanaendelea nchini Iraq

Rais Fuad Masum wa Iraq na ujumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Kurdisan leo wameitisha kikao cha kujadili uchaguzi wa hivi karibuni wa nchi hiyo na njia za kushirikiana makundi ya Kikurdi na mirengo mingine bungeni.

Ujumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Kurdistan ya Iraq ambao umeelekea mjini Baghdad kufanya mazungumzo na mirengo mingine ya kisiasa kwa ajili ya kuunda serikali mpya nchini humo umeonana pia na Nouri al Maliki, mkuu wa Muungano wa Serikali ya Kisheria na wamejadiliana njia za kuondoa tofauti ndogondogo na kuleta maelewano mapya.

Ujumbe huo wa Umoja wa Kitaifa wa Kurdistan ya Iraq umeonana pia na Muqtada al Sadr, mkuu wa muungano wa Sairun na Haydar al Abadi, Waziri Mkuu wa hivi sasa wa Iraq. Aidha umeonana na Ammar al Hakim na Usama al Najifi wa mirengo mingine mikubwa ya kisiasa nchini Iraq.

Rais Fuad Masum wa Iraq

 

Jana usiku pia Rais Fuad Masum wa Iraq alionana na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Nouri al Maliki ambaye pia ni mkuu wa muungano wa Serikali ya Kisheria katika bunge la Iraq na walijadiliana matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge na masuala ya kisiasa na kiusalama ya Iraq na ya eneo zima la Mashariki ya Kati.

Uchaguzi wa bunge ulifanyika nchini Iraq Jumamosi Mei 12, 2018 na kushirikisha karibu Wairaq milioni 11 ambao ni zaidi ya asimilimia 44 ya watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kura nchini humo.