Wazayuni waendelea kuwaua shahidi na kuwajeruhi Wapalestina
Kijana mmoja wa Palestina ameuawa shahidi huku watu wengine 109 wakijeruhiwa katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea' yaliyofanyika jana Ijumaa katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, aliyeuawa shahidi katika Ijumaa ya Tisa ya Maandamano ya Haki ya Kurejea hapo jana ni kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 24.
Habari zaidi zinasema kuwa, kijana huyo aliaga dunia kutokana na majeraha ya risasi, muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Quds, katika Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu.
Maafisa wa ngazi za juu wa harakati za mapambano za Hamas na Jihad Islami walishiriki maandamano ya jana na kulaani ukatili huo wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya waandamanaji ambao hawajajizatiti kwa silaha.
Maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa 'Siku ya Ardhi' na kwa ajili ya kupigania haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi.
Maandamano hayo yamekuwa yakikabiliwa kwa mkono wa chuma na wanajeshi katili wa Israel, ambapo kufikia sasa Wapalestina 116 wameshauawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi hao dhalimu na karibu 13,000 wengine kujeruhiwa.