Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Misri atiwa mbaroni
(last modified Mon, 28 May 2018 04:16:31 GMT )
May 28, 2018 04:16 UTC
  • Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Misri atiwa mbaroni

Vyombo vya usalama vya Misri vimemtia mbaroni kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo, Hazim Abdelazim.

Ijapokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani haijaeleza sababu za kukamatwa mwanasiasa huyo wa upinzani, lakini vyanzo vya habari vimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Hazim Abdelazim amekamatwa kutoka nyumbani kwake viungani mwa mji mkuu Cairo, kwa tuhuma za kuchapisha habari za uongo na kueneza uchochezi dhidi ya dola.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Misri yamesema kukamatwa kwa kingozi huyo wa upinzani ni muendelezo wa ukandamizaji na mbinyo wanaowekea wapinzani na wakosoaji wa serikali nchini humo.

Februari mwaka huu, mkuu wa chama cha upinzani cha Misri Imara, Abdul Moneim Aboul Fotouh alitiwa mbaroni baada ya kutoa mwito wa kususiwa uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Machi, kulalamikia hatua ya Rais Abdul Fattal al-Sisi ya kumkandamiza kila aliyetangaza nia ya kuchuana naye kwenye uchaguzi huo.

Baadhi ya wanahakarakati wanaozuiliwa nchini Misri

Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilidai kuwa, Aboul Fotouh alikamatwa kutokana na kuwa na uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin na kupanga njama za kuchochea machafuko nchini Misri.

Wanasiasa wengine kadhaa walikamatwa baada ya kutangaza azma yao ya kuchuana na al-Sisi katika uchaguzi huo wa Machi.

Tags