Kundi la kigaidi la al-Qaeda lamuonya vikali Bin Salman
Kundi la kigaidi la al-Qaeda katika Peninsula ya Kiarabu (AQAP) limemuonya vikali Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme nchini Saudi Arabia kutokana na kile linachokitaja kuwa 'miradi yake miovu'.
Kundi hilo la kitakfiri lenye makao yake huko Yemen limesema, "enzi mpya ya Bin Salman ya kufufua kumbi za senema kuchukua pahala pa misikiti kutafungua milango ya kuenea ufisadi na mmomonyoko wa maadili."
Kundi hilo la kigaidi linaamini kuwa, mabadiliko mapya yaliyotangazwa na Bin Salman ndani ya Saudia yanatishia misingi ya aidiolojia ya Uwahhabi, inayofuatwa na magenge ya kitakfiri duniani.
Kundi la kigaidi la al-Qaeda katika Peninsula ya Kiarabu limedai kuwa, mienendo hiyo ya Bin Salman ya kujaribu 'kukumbatia umagharibi' kama vile kuruhusu kufunguliwa kumbi za senema na kuwaruhusu wanawake kuendesha magari haipaswi kuvumiliwa kabisa.
Aidha genge hilo la kitakfiri limemkosoa vikali Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia kwa kuruhusu kufanyika mchezo wa mieleka ya WWE Royal Rumble mwezi Aprili mwaka huu mjini Jeddah, ambapo wanamieleka mashuhuri wa Marekani walishiriki.
Kwa mujibu wa AQAP, wanamieleka hao walikuwa wamebeba nembo za misalaba, mbali na kupigana wakiwa nusu uchi mbele ya mkusanyiko wa vijana wa kike na kiume wa Kiislamu.
Aidha wamemkosoa vikali Bin Salman kwa kuruhusu kufanyika matamasha ya miziki katika nchi hiyo yenye miji na maeneo matakatifu ya Kiislamu.