Maandamano yachachamaa Jordan, Waziri Mkuu alazimika kujiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45406-maandamano_yachachamaa_jordan_waziri_mkuu_alazimika_kujiuzulu
Waziri Mkuu wa Jordan amelazimika kujiuzulu kufuatia maandamano ya siku kadhaa ya wananchi, kulalamikia sera za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 04, 2018 09:57 UTC
  • Maandamano yachachamaa Jordan, Waziri Mkuu alazimika kujiuzulu

Waziri Mkuu wa Jordan amelazimika kujiuzulu kufuatia maandamano ya siku kadhaa ya wananchi, kulalamikia sera za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo.

Hani al-Mulki amewasilisha barua yake ya kujiuzulu baada ya kukutana na Mfalme Abdullah wa Pili wa nchi hiyo katika mji mkuu Amman leo Jumatatu, ikiwa ni katika jitihada za kujaribu kuwatuliza wananchi wa nchi hiyo, ambao wamekuwa wakifanya maandamano nyakati za usiku kwa siku siku kadhaa sasa.

Mfalme wa nchi hiyo amemuomba Omar al-Razzaz, mchumi wa zamani wa Benki ya Dunia kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi na al-Mulki na kumtaka atangaze serikali mpya.

Mfalme Abdullah wa Jordan (Kulia) na Waziri Mkuu aliyejiuzulu

Waandamanaji hao wamewakosoa vikali wanasiasa wanaofuja fedha za umma huku wakipandisha kodi kwa wananchi walalahoi. Wamesema katu hawawezi tena kuvumilia kiwango cha ufisadi kinachoshuhudiwa nchini humo, huku wakimtaka Mfalme Abdullah wa Pili kuingilia kati.

Polisi ya Jordan imesema kuwa imewatia mbaroni watu 60, kwa kuvunja sheria wakati wa maandamano hayo. Aidha maafisa usalama 42 wamejeruhiwa katika maandamano hayo.

Kwa mujibu wa takwimu tasmi za serikali, asilimia 18.5 ya wananchi milioni 9.5 wa Jordan hawana ajira, huku asilimia 20 wakiwa katika ncha ya umaskini wa kupindukia.