Tamko la kinagaubaga la Assad; uhusiano wa Iran na Syria haurubuniki
Rais wa Syria amesema kuhusu pendekezo la Saudi Arabia la kuirubuni nchi hiyo ivunje uhusiano wake na Iran na kuwa tayari kuipatia hongo serikali ya Damascus kwamba: "Si Syria wala si Iran ambayo inatangaza mnada kuhusu uhusiano huu katika soko la kisiasa la kimataifa hata pahitajike mahali pa kufanyia muamala huo."
Rais Bashar al-Assad wa Syria ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya Al-Alam na kufafanua kuwa: "Uhusiano wa kistratejia wa Iran na Syria hauathiriwi na masuala ya kusini na kaskazini; hakika ya uhusiano huu na hali zake zote inafungamana na hali ya sasa na ya mustakabali ya eneo wala hauathiriwi na bei za soko la kimataifa."

Kuhusu kuwepo kwa vikosi vya Iran nchini Syria pia, Rais Bashar Al-Assad ameyazima makelele ya propaganda yaliyoenezwa hivi karibuni kwa kusema: "Tokea mwanzo, serikali ya Syria ilizitaka Iran na Russia ziwepo nchini Syria kwa sababu ilihitaji msaada wa nchi hizo; na Iran ikaitikia ombi lililotolewa na Syria.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ni nchi yenye ushirikiano wa kistratejia na Syria, wakati ulipoanza mgogoro wa nchi hiyo ilitangaza utayari wa kuisaidia Damascus. Kuwa bega kwa bega Iran na serikali halali ya Syria mara baada ya kuanza vita vya niaba vilivyoanzishwa na magaidi wa kukodiwa, kulibadilisha kikamilifu matukio ya kwenye medani za vita na mlingano wa kisiasa ndani ya nchi hiyo. Leo hii kwa baraka za ushirikiano wa kistratejia wa mhimili wa Muqawama nchini Syria, nafasi ya magaidi kujifaragua imefinyika mno; na kwa sababu hiyo waungaji mkono wao wanatafuta njia za kujivua na dhima hiyo sambamba na kupiga upatu wa kujaribu kuutia doa na ila uwepo na ushawishi athirifu wa kieneo wa Iran. Madai yasiyo na msingi wowote ya rais wa Marekani Donald Trump kwamba Iran ina nafasi hasi na haribifu katika eneo, madai ambayo yanatolewa kwa madhumuni ya kuishinikiza Tehran; na vilevile makelele ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu mchango wa Iran nchini Syria, yote hayo yanaashiria mabadiliko ya mlingano wa nguvu za kisiasa katika eneo kwa manufaa ya mhimili wa muqawama. Mabadiliko makubwa yanayojiri kwenye medani za vita nchini Syria bila shaka yanatokana na mchango wenye taathira uliotolewa na mhimili wa muqawama, ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo pia imegharimika katika suala hilo. Kuwepo kwa washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria kumekuwa na athari kwa kiwango ambacho katika mahojiano na kanali na Al-Alam, Rais Bashar Al- Assad amekutolea ufafanuzi maridhawa kwa kusema: "Iran imepigana vita kuwalinda wananchi wa Syria, na imejitolea hivyo kwa damu yake pia; kwa hivyo kutumia neno washauri maana yake ni kwamba Iran haina kituo cha kijeshi na kivita nchini Syria."

Lakini mbali na hayo; utawala wa Kizayuni unashirikiana na makundi yanayobeba silaha na ya kigaidi katika eneo la Golan unalolikalia kwa mabavu. Ushirikiano wao umefikia kiwango cha kuunda kamati ya pamoja ya utendaji; hii ikiwa na maana kwamba makundi yanayobeba silaha na ya kigaidi yametoa ahadi ya kutoishambulia Israel na mkabala wake yatapatiwa na utawala huo wa Kizayuni huduma za matibabu kwa ajili ya majeruhi wao pamoja na dawa, chakula, silaha na zana za kivita. Sera hii ya Wazayuni imelifanya eneo la kusini magharibi mwa Syria liwe na umuhimu maradufu. Hivi sasa ambapo jeshi la Syria limetangaza kuwa limekusudia kuyakomboa maeneo yote ya kusini mwa nchi hiyo, wasiwasi wa Israel kuhusu hatima ya makundi yanayobeba silaha na ya magaidi umezidi kuongezeka. Makelele ya uropokaji yanayopigwa na waziri mkuu wa Israel kuhusu nafasi ya Iran nchini Syria yanaweza kutathminiwa katika muelekeo huo. Lakini kama alivyosisitiza Rais Assad ni kwamba licha ya uungaji mkono wa Israel kwa magaidi, Syria imetekeleza wajibu wake, hivyo haijalishi kama Israel inaafiki au haiafiki, kwa sababu jeshi la Syria linapigana vita katika medani ya kusini, na huo ndio uamuzi ulioamuliwa kuchukuliwa na nchi hiyo.../