Jun 17, 2018 15:02 UTC
  • Haaretz: Ni Israel ndiyo iliyoangamiza uchumi wa Ukanda wa Ghaza

Gazeti la utawala wa Kizayuni la Haaretz limeandika kuwa, Israel ndiyo iliiyoangamiza uchumi wa Ukanda wa Ghaza kutokana na mashambulizi yake ya mara kwa mara kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na zana za uvuvi za wananchi hao wa Ghaza.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, katika hali ambayo karibu asilimia 90 ya wakazi wa Ghaza wanaishi chini ya mstari wa umaskini, sekta ya uvuvi ni muhimu mno kwa wakazi wa eneo hilo, lakini hata hivyo, Israel haiwaruhusu wavuvi wa Kipalestina kujitafutia riziki zao kupitia uvuvi.

Njia kuu ya kuendeshea maisha ya wananchi wa Ghaza ni uvuvi, lakini Israel inawashambulia kwa risasi mara kwa mara wananchi hao madhlumu

Limeendelea kuandika, wavuvi wa Kipalestina wakazi wa Ghaza ambao wanategemea uvuvi kujiokoa na kifo cha njaa, wanashambuliwa mara kwa mara na wanajeshi wa Israel kiasi kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mamia ya wavuvi wa Kipalestina wameuliwa kwa risasi za wanajeshi wa Israel katika fukwe za mashariki mwa bahari ya Mediterranean zinazopakana na ukanda huo.

Mwandishi wa habari hiyo ameongeza kuwa, jeshi la majini la Israel limeweka vizuizi vingi vya kuwazuia wavuvi wa Palestina kuendesha shughuli ya uvuvi baraharini. Sekta ya uvuvi ya wakazi wa Ghaza imekufa kiasi kwamba ni karibu wavuvi elfu tatu na mia saba tu wa Kipalestina ndio walioandikisha majina yao katika Jumuiya ya Wavuvi wa Palestina wakati ambapo mwaka 2000 idadi ya wanachama wa jumuiya hiyo walikuwa karibu elfu kumi.

Gazeti la Haaretz pia limeandika, jeshi la Israel limepiga marufuku kuwafikia Wapalestina vipuri vya kutengenezea boti zao za uvuvi zinapoharibika ikiwa ni muendelezo wa kulifungia eneo la Ghaza njia zote za ardhini, angani na baharini.

Sekta ya uvuvi ni muhimu sana kwa uchumi wa Ghaza, lakini Israel hairuhusu wakazi wa ukanda huo kutumia haki yao hiyo ya kimsingi

 

Tags