Rais wa Afghanistan aliamuru jeshi kuanza tena mashambulizi dhidi ya Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46478-rais_wa_afghanistan_aliamuru_jeshi_kuanza_tena_mashambulizi_dhidi_ya_taliban
Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ametangaza rasmi mwisho wa usitishaji wa mapigano dhidi ya kundi la Taliban na kuliamuru jeshi la nchi hiyo kuanza tena mashambulizi dhidi ya kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2018 11:53 UTC
  • Rais wa Afghanistan aliamuru jeshi kuanza tena mashambulizi dhidi ya Taliban

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ametangaza rasmi mwisho wa usitishaji wa mapigano dhidi ya kundi la Taliban na kuliamuru jeshi la nchi hiyo kuanza tena mashambulizi dhidi ya kundi hilo.

Ghani liyekuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Kabul amelitaka pia kundi la Taliban kujiunga na mchakato wa mazungumzo ya amani baada ya usitishaji mapigano wa siku 18 kote nchini Afghanistan.

Amesema usitishaji vita huo umefanikiwa kwa asilimia 98 na kwamba wapiganaji wengi wa kundi la Taliban na raia wanataka amani.

Wito huo wa Rais wa Afghanistan umetolewa baada ya kundi la wanaharakati wa amani wa Kiafghani kutembea kwa miguu kutoka mkoa wa Helmand hadi Kabul wakizitaka pande zombe mbili kukomesha mapigano nchini humo.

Wapiganaji wa kundi la Twaliban

Hata hivyo kundi la Taliban limekataa wito wa kufanya mazungumzo na serikali ya Kabul na kuendeleza mapigano na hujuma kali katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan.

Siku chache zilizopita kundi hilo la Twaliban lilishambulia ghafla kituo cha polisi katika mkoa wa Badghis ulioko magharibi mwa nchi hiyo na kuua polisi wasiopungua 30.