Ndege za kijeshi za Iraq zaangamiza magaidi 30 wa Daesh, Salahuddin
Ndege za kijeshi za Iraq zimefanya mashambulizi ya anga na kufanikiwa kuangamiza wanachama wasiopungua 16 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, katika mkoa wa Salahuddin.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Iraq imesema kuwa, magaidi hao waliuawa katika operesheni iliyolenga maficho ya mabaki ya magaidi hao wakufurishaji katika eneo la Tal Farhan, katikati ya mji wa Tuz Khurmatu, umbali wa maili 55 kusini mwa Kirkuk.
Wakati huo huo, duru za kijasusi zimearifu kuwa, wanachama wengine 14 wa genge hilo la kitakfiri wameuawa katika operesheni nyingine tofauti kaskazini mwa mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Kirkuk.
Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq hivi karibuni alisisitizia ulazima wa kudhaminiwa usalama wa mipaka ya nchi hiyo na kufanyika operesheni dhidi ya wafuasi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ndani na nje ya mipaka ya Iraq.
Kufuatia kushindwa vibaya kundi la Daesh nchini Iraq na Syria, wanachama wa kundi hilo waliosambaratika wameweka kambi katika mipaka ya nchi hizo suala ambalo limeyafanya majeshi ya nchi hizo (Iraq na Syria) kuanzisha operesheni kabambe kwa ajili ya kuyasafisha maeneo hayo ya mipakani.