Jeshi la Israel lashambulia maandamano ya wanawake wa Kipalestina, 134 wajeruhiwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46553-jeshi_la_israel_lashambulia_maandamano_ya_wanawake_wa_kipalestina_134_wajeruhiwa
Askari katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameyashambulia kwa risasi hai maandamano ya wanawake wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kujeruhi 134 miongoni mwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2018 02:57 UTC
  • Jeshi la Israel lashambulia maandamano ya wanawake wa Kipalestina, 134 wajeruhiwa

Askari katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameyashambulia kwa risasi hai maandamano ya wanawake wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kujeruhi 134 miongoni mwao.

Ashraf al-Qudra, msemaji wa Wizara ya Afya ya Gaza amesema kuwa, waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia maandamano hayo ya jana Jumanne ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa vibaya.

Maandamano hayo ya jana ndiyo yaliyokuwa makubwa zaidi kuwahi kuitishwa na wanawake wa Kipalestina, tangu yaanze maandamano ya 'Haki ya Kurejea' mnamo Machi 30 mwaka huu katika Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro wa kidhalimu.

Rim Abu Irmana, mmoja wa waandamanaji hao amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, "Haya ni maandamano ya amani ya kupigania haki zetu na ardhi yetu. Nimekuja kumalizia kile alichoanzisha binti yangu wa miaka 15, kwa jina Wasal Irmana, aliyeuawa kwa risasi za jeshi katili la Israel katika maandamano ya Mei 15."

Licha ya kuuawa wenzao, Wapalestina wameshikilia kuwa hawatosalimu amri mbele ya unyama wa Israel

Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 140 wameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel kwenye maandamano hayo na wengine zaidi ya elfu 15 wamejeruhiwa.

Maandamano ya 'Haki ya Kurejea' yalianza tarehe 30 mwezi Machi, kushinikiza kurejea kwa wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao zilizoghusubiwa na walowezi wa Kiyahudi.