Shambulizi la kigaidi Balochistan, nchini Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46770-shambulizi_la_kigaidi_balochistan_nchini_pakistan
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulizi la kigaidi lililolenga mkutano wa kampeni za uchaguzi katika mkoa wa Balochistan nchini Pakistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2018 07:23 UTC
  • Shambulizi la kigaidi Balochistan, nchini Pakistan

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulizi la kigaidi lililolenga mkutano wa kampeni za uchaguzi katika mkoa wa Balochistan nchini Pakistan.

Bahmar Qassemi amekemea vikali shambulio hilo na kutuma salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Pakistan na vilevile familia za wahanga wa shambulizi hilo. 

Shambulizi hilo la kigaidi lililenga mkusanyiko wa kampeni za uchaguzi za chama cha Balochistan Awami (BAP) katika eneo la Mastung kwenye jimbo la Balochistan kusini magharibi mwa Pakistan na limeua watu wasiopungua 130 akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Nawabzada Siraj Raisani aliyekuwa akigombea kiti cha bunge la eneo hilo. Watu wengine 150 wamejeruhiwa. 

Zaidi ya watu 120 wameuawa Balochistan, Pakistan

Shambulizi hilo la kigaidi ambalo kundi la Daesh limetangaza kuwa ndilo lililolipanga na kulitekeleza, ndilo kubwa zaidi la kundi hilo la kigaidi nchini Pakistan. Pamoja na hayo na kwa kutilia maanani ushindani mkali wa vyama na makundi mbalimbali na vilevile utitiri wa makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha na makundi ya kigaidi katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan hususan yale yanayotaka kujitenga, inakuwa vigumu kuweza kusema kuwa shambulizi hilo limefanywa na kundi la Daesh. Hii ni pamoja na kuwa serikali ya Pakistan inapinga madai kuwa kundi la Daesh linaendesha harakati zake nchini humo. Vilevile baadhi ya makundi yanayotaka kujitenga eneo la Balochistan hayapendi kuona vyama vya siasa vikishiriki katika kampeni za uchaguzi wa mabunge na mabaraza ya Pakistan na yanaamini kuwa, kufanya hivyo ni kuunga mkono utawala wa Islamabad katika jimbo hilo; kwa msingi huo yamekuwa yakishambulia mikutano na vikao vya kampeni za uchaguzi. Wakati huo huo muungano wa makundi ya kiwahabi na kitakfiri ya Pakistan kama lile linalojiita Jeshi al Sahaba au Lashkar-e-Jhangvi na genge la kigaidi la Daesh umetatiza sana hali ya usalama nchini Pakistan. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, makundi hayo yamekuwa yakifanya mashambulizi ya kigaidi kwa jina la kundi la Daesh.

Shambulizi la Balochistan limelenga mkutano wa kampeni za uchaguzi

Rahiim Yusuf Zay ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Pakistan anasema: Kundi la Daesh limepata ushawishi nchini Afghanistan lakini bado ni dhaifu huko Pakistan. Kundi la Twaliban la Pakistan na makundi mengine yenye misimamo mikali yaliyojiunga na Daesh yamelazimika kukimbilia Afghanistan au kwenda mafichoni kutokana na operesheni na jeshi la Pakistan; suala hilo linayalazimisha makundi hayo kufanya mashambulizi ya kuvizia katika maeneo mbalimbali ya Pakistan."

Lengo muhimu zaidi la makundi hayo ya kigaidi na Daesh ni kushambulia maeneo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na kuchochea hitilafu za kidini na kimadhehebu nchini humo. Kwa sasa makundi hayo yameelekeza mashambulizi yao katika maeneo ya kikaumu na kikabila kama Balochistan na jimbo la Khyber Pakhtunkhwa na yanajitengenezea maficho salama kupitia njia ya kushambulia na kuchafua amani na usalama wa maeneo mbalimbali ya Pakistan.

Shambulizi la kigaidi Mastung, Pakistan

Kwa vyovyote vile shambulizi la kigaidi dhidi ya mkutano wa kampeni za uchaguzi katika jimbo la Balochistan, bila ya kujali limetekelezwa na nani, ni kielelezo cha kuendelea hali ya ukosefu wa amani nchini Pakistan. Shambulizi hilo linazidisha udharura wa kuwepo ushirikiano mkubwa baina ya nchi za eneo hilo kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi na kuacha kutumia makundi hayo kama wenzo wa kutimizia malengo mbalimbali ya kisiasa.