Hamas yaionya vikali Israel juu ya mzingiro wa Gaza
(last modified Tue, 17 Jul 2018 07:17:41 GMT )
Jul 17, 2018 07:17 UTC
  • Hamas yaionya vikali Israel juu ya mzingiro wa Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel, kutokana na hatua yake ya kuzidisha mzingiro katika Ukanda wa Gaza.

Fawzi Barhumi, msemaji wa Hamas ameitaja hatua ya Israel ya kufunga kivuko muhimu cha Kerem Shalom kuwa jinai dhidi ya Wapalestina, huku akiuonya vikali utawala huo juu ya matokeo mabaya ya kitendo chake hicho.

Kufungwa kwa kivuko hicho katika mji wa Rafah kutazuia kuingizwa katika eneo la Gaza bidhaa za msingi zikiwemo za fueli, dawa na vifaa vya ujenzi. 

Hata hivyo Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman amedai kuwa, njia hiyo muhimu itafungwa kuanzia leo Jumanne hadi Jumapili ijayo ili kuzuia kuingizwa mafuta na gesi pekee katika ukanda huo, na kuwa eti chakula na dawa zitaruhusiwa.

Kivuko cha Rafah

Lieberman amesema utawala huo haramu umechukua hatua hiyo ili kujibu kile anachodai kuwa ni 'njama za kigaidi' za Hamas. 

Tangu Januari mwaka 2006 na kufuatia ushindi wa harakati ya Hamas katika uchaguzi wa Bunge la Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel uliliwekea eneo la Ukanda wa Gaza mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa lengo la kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama. Hata hivyo njama hizo hazijazaa matunda kufikia sasa. 

Tags