Indhari ya Unicef kuhusu hali ya mgogoro huko Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46868-indhari_ya_unicef_kuhusu_hali_ya_mgogoro_huko_yemen
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza kuwa kuendelea mapigano huko Yemen kunazifanya ngumu shughuli za utoaji misaada ya kibinadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 19, 2018 03:06 UTC
  • Indhari ya Unicef kuhusu hali ya mgogoro huko Yemen

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza kuwa kuendelea mapigano huko Yemen kunazifanya ngumu shughuli za utoaji misaada ya kibinadamu nchini humo.

Unicef jana ilitahadharisha kuwa kuendelea mapigano na kuwepo matatizo katika mifumo ya afya, kunatatiza shughuli za viongozi wa kieneo na za taasisi za utoaji misaada za kimataifa. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonegza kuwa viongozi wa kieneo huko Yemen na taasisi za kimataifa zinazohusika na misaada ya kibinadamu zimekuwa zikifanya jitihada za kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo. 

Kuenea maradhi ya kipindupindu huko Yemen 

Kabla ya hapo, Henrietta Fore Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef alilaani kuendelea mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen na kueleza kuwa watoto wa Kiyamani 2200 wameuawa hadi kufikia sasa tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Aal Saudi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Afisa huyo wa Unicef ameongeza kuwa idadi kubwa ya watoto wa Kiyamani wanakabiliwa na njaa au wanalazimika kushiriki vitani. Amesema watoto hao wanakabiliwa na hatari ya kuaga dunia kutokana na kuugua maradhi ambayo yanaweza kuzuilika. 

Shirika la Afya Duniani (WHO)  pia limetangaza kuwa hali ya kiafya katika mji wa al Hudaydah magharibi mwa Yemen ni dhaifu na ya kusikitisha na kwamba hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuwadhaminia mahitaji wakazi wa mji huo ambao wanahitaji zaidi huduma za msingi khususan akinamama, watoto na wagonjwa.