Magaidi saba wa ISIS wapata kifungo cha maisha gerezani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46909-magaidi_saba_wa_isis_wapata_kifungo_cha_maisha_gerezani
Mahakama nchini Iraq imewahukumu vifungo vya maisha gerezani magaidi saba Wairaqi wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh baada ya kuwapata na hatia ya kusaidia katika utekelezaji wa hujuma za kigaidi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 21, 2018 01:18 UTC
  • Magaidi saba wa ISIS wapata kifungo cha maisha gerezani

Mahakama nchini Iraq imewahukumu vifungo vya maisha gerezani magaidi saba Wairaqi wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh baada ya kuwapata na hatia ya kusaidia katika utekelezaji wa hujuma za kigaidi nchini humo.

Abdul Sattar al-Biraqdar, Msemaji wa Baraza Kuu la Mahakama Iraq amesema Mahakama Kuu ya Jinai nchini humo imetoa hukumu hizo baada ya magaidi hao kukiri kuwa walitoa msaada wa kilogistiki kwa ISIS na kutoa mchango katika hujuma dhidi ya vikosi vya usalama.

Mnamo Julai 8,  Mahakama ya Jinai Mkoani Nineveh ilitoa hukumu ya kifo dhidi ya magaidi wa ISIS waliopatikana na hatia ya kuwaua watu 16 katika Hospitali Kuu ya Mosul, kaskazini mwa Iraq.

Magaidi wa ISIS

Mwezi Aprili Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi alisisitiza kuwa, kwa kutegemea umoja na mshikamano wake na uwezo wa wapiganaji na wanachi wake, Iraq haitaruhusu magaidi wa ISIS warudi tena nchini humo.

Desemba 2017, al-Abadi, alitangaza rasmi kukombolewa ardhi yote ya nchi hiyo kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS ambao walikuwa wameteka eneo kubwa la nchi hiyo mwaka 2014.