Walowezi 1000 wa Kizayuni wakishambulia tena kibla cha kwanza cha Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46943-walowezi_1000_wa_kizayuni_wakishambulia_tena_kibla_cha_kwanza_cha_waislamu
Kwa mara nyingine tena walowezi zaidi ya 1000 wa Kizayuni wameuhujumu Msikiti wa al Aqsa ulioko katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 22, 2018 13:57 UTC
  • Walowezi 1000 wa Kizayuni wakishambulia tena kibla cha kwanza cha Waislamu

Kwa mara nyingine tena walowezi zaidi ya 1000 wa Kizayuni wameuhujumu Msikiti wa al Aqsa ulioko katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Shirika la habari la Safa linalorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu limeandika kuwa, Wazayuni hao wamefanya hujuma hiyo na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu, huku wakiwa wanapewa ulinzi kamili na wanajeshi na maafisa wa polisi wa utawala haramu wa Israel.

Walowezi hao wa Kiyahudi wameyavamia matukufu hayo ya Kiislamu kwa kisingizio cha kuadhimisha 'Sikukuu' ya Mayahudi inayoitwa Tisha B’Av.

Duru za habari zinaarifu kuwa, walowezi hao wa Kizayuni mapema leo Jumapili waliuhujumu Msikiti wa al Aqsa kupitia mlango wa Bab al-Magharibah huku wakiwa wamepewa ulinzi wa vikosi maalumu vya polisi na jeshi la Israel.

Masjidul Aqsa, Kibla cha kwanza cha Waislamu

 

Ardhi za Palestina zinashuhudia hali ya taharuki kubwa tokea Rais wa Marekani Donald Trump atangaze Disemba mwaka jana kuwa ameitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.

Kitendo hicho cha Marekani kuuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds, kiliibua hasira za Wapalestina na Waislamu kote duniani mbali na kulaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.