Malaysia yaitaka dunia kupambana na utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46982-malaysia_yaitaka_dunia_kupambana_na_utawala_wa_kizayuni
Serikali ya Malaysia imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na sheria iliyopasishwa na utawala haramu wa Kizayuni juu ya kuundwa nchi ya Kiyuhudi katika ardhi za Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 24, 2018 07:56 UTC
  • Malaysia yaitaka dunia kupambana na utawala wa Kizayuni

Serikali ya Malaysia imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na sheria iliyopasishwa na utawala haramu wa Kizayuni juu ya kuundwa nchi ya Kiyuhudi katika ardhi za Palestina.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia sambamba kulaani kupasishwa hivi karibuni sheria hiyo ya kibaguzi katika bunge la utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuundwa kile kinachoitwa kuwa nchi ya Kiyahudi, imesema kuwa, jamii ya kimataifa ni lazima ichukue hatua za haraka kwa kuutaka utawala huo kuhitimisha mara moja sheria na siasa za kibaguzi na ukandamizaji dhidi ya taifa la Palestina. Kadhalika taarifa hiyo imesisitiza kwamba, kupasishwa  sheria hiyo, ni njama ambayo itadhoofisha na kuharibu azimio kamili na jumuishi katika kutatua mgogoro wa Palestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia imezidi kufafanua kuwa, sheria ambayo inazitaja ardhi za Palestina kuwa ni mali ya Wazayuni, ni ya kibaguzi na kwa msingi huo, serikali ya Kuala Lumpur itaendelea kuunga mkono sheria yoyote inayoitambua Palestina na mji mkuu wake ukiwa ni Quds. 

Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa kibaguzi wa Israel

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) zinachukuliwa kuwa ni za Mayahudi pekee na kwamba Wapalestina wanaoishi katika ardhi hizo watanyimwa haki zote za kiraia na za kibinadamu. Vilevile lugha ya Kiibrania ndiyo itakayokuwa lugha rasmi katika ardhi hizo. Sheria hiyo licha ya kuutambua mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala huo ghasibu, inatambua ujenzi na kupanuliwa kwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kuwa thamani ya kitaifa na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuimarisha vitongoji vilivyopo sasa na kujengwa vingine vipya.