Harakati ya Fat-h yaafiki mpango wa maridhiano ya kitaifa
Mjumbe wa kamati kuu ambaye pia ni mkuu wa kamati ya ufuatiliaji maridhiano ya kitaifa wa harakati ya Fat-h amesema harakati hiyo imetoa jibu chanya la maandishi kwa maafisa wa Misri kuhusiana na mapendekezo yaliyowasilishwa na nchi hiyo kuhusu maridhiano ya kitaifa ya Palestina.
Azzam Ahmad amesema, jibu la Fat-h limewasilishwa kwa Waziri wa Usalama wa Misri Abbas Kamel na kuongeza kuwa, mpango huo unatokana na mapatano ya kitaifa yaliyosainiwa mwaka 2011 na kwamba makubaliano yaliyofikiwa yataingia kwenye hatua ya utekelezaji hivi karibuni.
Awali Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS alisema kupitia mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Usalama wa Misri kuwa, kwa kuzingatia mazingira maalumu yanayotawala katika kadhia ya Palestina hususan kuhusu Quds na wakimbizi Wapalestina, harakati hiyo imeafiki mpango mpya wa maridhiano ya kitaifa uliopendekezwa na Misri.
Kwa mujibu wa Mousa Abu Marzouq, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, mapendekezo muhimu zaidi yaliyowasilishwa na Misri katika mpango huo mpya wa maridhiano ya kitaifa ya Palestina yanajumuisha kusimamishwa adhabu zinazotekelezwa dhidi ya Ukanda wa Gaza, kufanyika uchaguzi wa Palestina bila masharti yoyote na kuanza mashauriano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Hapo kabla mnamo tarehe 12 Oktoba 2017, harakati za Fat-h na Hamas zilitia saini maridhiano ya kitaifa mjini Cairo, Misri.../