Hamas yataka kuendeleza maandamano ya Kurejea
(last modified Fri, 10 Aug 2018 16:19:59 GMT )
Aug 10, 2018 16:19 UTC
  • Hamas yataka kuendeleza maandamano ya Kurejea

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas amesisitiza kuwa wananchi wa Palestina wataendelea kufanya maandamano makubwa ya "Haki ya Kurejea" hadi pale malengo yao yatakapofanikishwa na kuvunjwa mzingiro wa Ghaza.

Hazim Qassim amesema leo Ijumaa katika mkutano na waandishi wa habari kuwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza kwa mara nyingine tena wameelekea katika eneo la mpakani mwa ukanda huo na kukabiliana na adui kwa  kushiriki katika maandamano hayo.  

Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa wananchi wa Palestina wana ari kubwa ya kuendeleza mapambano dhidi ya Wazayuni maghasibu hadi watakapokuwa huru na kujitawala. 

Kamati ya kitaifa inaoandaa maandamano ya Haki ya Kurejea na kuvunja mzingiro umewataka wananchi wa Palestina kushiriki kwa wingi katika maandamano makubwa ya leo katika maeneo mbalimbali ya mpaka wa Ghaza na  ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Vijana wa Kipalestina katika maandamano ya kila Ijumaa ya haki za kurejea

Maandamano hayo ya Haki ya Kurejea, Ijumaa hii yamefanyika kwa anwani ya "Ijumaa ya Uhuru na Maisha." Maandamano hayo yanayofanyika katika Ukanda wa Ghaza kila Ijumaa yalianza tarehe 30 Machi na hadi kufikia sasa Wapalestina zaidi ya 150 wameuawa kwenye maandamano hayo kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel, na karibu elfu 18 wamejeruhiwa. 

Tags