Malaysia yasitisha kikamilifu ushirikiano na Saudia katika vita dhidi ya Yemen
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa nchi yake imesitisha uhusiano wa aina zote na Saudi Arabia katika vita vya nchi hiyo dhidi ya taifa la Yemen.
Mahathir Muhammad ametangaza kuwa Malaysia haitaki kuhusishwa na vita na jinai zinazofanywa na Saudi Arabia huko Yemen. Ameongeza kuwa, Kuala Lumpur itajiepusha na harakati yoyote inayoweza kuifanya Malaysia ituhumiwe kuwa inatumia mabavu.
Ushindi wa Mahathir Muhammad katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika hivi karibuni nchini Malaysia umetoa pigo kubwa kwa sera na siasa za Saudi Arabia katika eneo al kusini mashariki mwa Asia kwa kadiri kwamba, Wizara ya Ulinzi ya Malaysia ilitangaza hivi karibuni kuwa, imefunga shughuli zote za mradi uliopewa jina la Kituo cha Amani cha Mfalme Salman kilichoanza kazi miezi 14 iliyopita wakati wa uwaziri mkuu wa Najib Tun Razak. Waziri huyo mkuu wa zamani wa Malaysia aliyekuwa na uhusiano mkubwa na wa karibu sana na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, anakabiliwa na kesi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma kwa kushirkiana na watala wa Aal Saud.

Suala hilo limewakasirisha sana wananchi wa Malaysia. Wizara ya Ulinzi ya Malaysia ilikuwa tayari imetangaza kwamba, imesitisha ushirikiano wake na Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Hata hivyo sisitizo la Mahathir Muhammad kuhusu kadhia hiyo lililotolewa baada ya shambulizi la hivi karibuni lililofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya basi lililokuwa limebeba watoto nchini Yemen ambalo limelaaniwa na dunia nzima, linazingatiwa kuwa na umuhimu mkubwa.
T.J. S Jor ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa India anasema: "Mashambulizi ya jeshi la Saudi Arabia dhidi ya Yemen yaliyoanza mwaka 2015 yanaigharimu nchi hiyo dola milioni 200 kila siku, na kushindwa vibaya kwa watawala wa Saudia katika vita hivyo kumezitia aibu nchi zinazoshiriki katika muungano wa vita wa Aal Saudi dhidi ya watu wa Yemen."
Malaysia ni miongoni ma nchi muhimu na za viwanda katika ulimwengu wa Kiislamu na hapana shaka kuwa, sisitizo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bwana Mahathir Muhammad la kusitishwa uhusiano wake na Saudia kutokana na jinai zake huko Yemen ni wito unaozitaka nchi nyingine za Kiislamu zisimamishe ushirikiano wao na Saudia katika mauaji ya watu wa Yemen. Saudi Arabia imekuwa ikianzisha na kuasisi shule na vyuo vya kidini katika nchi mbalimbali na kufadhili harakati za kuhubiri mafundisho ya Kiwahabi na kitakfiri, na shule hizo zimekuwa zikilea na kutengeneza makundi ya watu wenye fikra na mitazamo ya kuchupa mipaka na ya kigaidi kama Daesh, Boko Haram na al Shabab.

Abbas Kara Aghachli ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Giresun nchini Uturuki anasema: "Mauaji yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen na uharibifu wa miundombinu ya nchi hiyo ni jinai dhidi ya binadamu inayoonesha kwamba, msingi wa utawala wa kifalme wa Saudia ni kuzusha mifarakano na migawanyiko. Inasikitisha kuona kwamba, jibu la jamii ya kimataifa kwa jinai zinazofanywa na Saudia ambayo ndiyo mlezi mkuubwa zaidi wa makundi ya kigaidi huko Yemen limeishia katika kulaani kwa maneno matupu na hadi sasa hakuna hatua yoyote ya kivitendo iliyochukuliwa kwa shabaha ya kukomesha mauaji ya watoto nchini Yemen."

Kwa vyovyote vile, baada ya ushindi wa Mahathir Muhammad huko Malaysia, ushindi wa Imran Khan katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Pakistan unatambuliwa kuwa ni pigo jingine kubwa kwa siasa za Saudi Arabia katika eneo hili. Agizo lililotolewa na mahakama ya Pakistan ikipinga ushirikiano wa Jenerali Raheel Sharif aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Nchi kavu la Pakistan na muungano eti wa kijeshi wa Saudia katika vita vya Yemen ni ithibati kwamba, mahakama na jeshi la Pakistan pia haziwezi kufumbia macho malalamiko makubwa ya raia wa nchi hiyo wanaopinga jinai na mauaji yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia huko Yemen.