Mahakama Iraq yawafunga maisha jela magaidi wa ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47859-mahakama_iraq_yawafunga_maisha_jela_magaidi_wa_isis
Mahakama nchini Iraq imewafunga kifungo cha maisha gerezani watu wanne ambao wamepatikana na hatia ya kujiunga na kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 03, 2018 02:42 UTC
  • Mahakama Iraq yawafunga maisha jela magaidi wa ISIS

Mahakama nchini Iraq imewafunga kifungo cha maisha gerezani watu wanne ambao wamepatikana na hatia ya kujiunga na kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh.

Sadeq al-Husseini, mkuu wa Kamati ya Usalama katika Baraza la Mkoa wa Diyala amesema mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya watu hao kupatikana na hatia ya kujiunga na ISIS na kusaidia kundi hilo katika hujuma dhidi ya maafisa wa usalama na wanajeshi.

Kufungwa magaidi hao ni katika sehemu ya mkakati wa kupambana na magaidi wa ISIS nchini Iraq.  Mnamo Agosti 19 Mahakama ya Iraq iliidhinisha kifungo cha maisha kwa magaidi zaidi ya 12 wa ISIS ambao walipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya Juni mwaka 2014 katika kituo cha ndege za kijeshi katika mkoa wa Salahuddin.

Julai 21 Mahakama nchini Iraq iliwahukumu vifungo vya maisha gerezani magaidi saba Wairaqi wa kundi la kigaidi la ISIS baada ya kuwapata na hatia ya kusaidia katika utekelezaji wa hujuma za kigaidi nchini humo. Aidha mnamo Julai 8,  Mahakama ya Jinai Mkoani Nineveh ilitoa hukumu ya kifo dhidi ya magaidi wa ISIS waliopatikana na hatia ya kuwaua watu 16 katika Hospitali Kuu ya Mosul, kaskazini mwa Iraq.

Magaidi wa ISIS

Mwezi Aprili Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi alisisitiza kuwa, kwa kutegemea umoja na mshikamano wake na uwezo wa wapiganaji na wanachi wake, Iraq haitaruhusu magaidi wa ISIS warudi tena nchini humo.

Desemba 2017, al-Abadi, alitangaza rasmi kukombolewa ardhi yote ya nchi hiyo kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS ambao walikuwa wameteka eneo kubwa la nchi hiyo mwaka 2014.