Uhispania: Marekani haina ustahiki wa kuwa mpatanishi katika kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47914-uhispania_marekani_haina_ustahiki_wa_kuwa_mpatanishi_katika_kadhia_ya_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema, Marekani imepoteza ustahiki wa kuwa msuluhishi katika suala la Palestina kutokana na kwenda sambamba na misimamo ya Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2018 03:30 UTC
  • Uhispania: Marekani haina ustahiki wa kuwa mpatanishi katika kadhia ya Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema, Marekani imepoteza ustahiki wa kuwa msuluhishi katika suala la Palestina kutokana na kwenda sambamba na misimamo ya Israel.

Josep Borrell ameyasema hayo mjini Madrid katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na waziri mwenzake wa Palestina Riyadh al-Maliki. Huku akiashiria hatua ya Marekani ya kukata misaada yake ya kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wakimbizi wa Palestina UNRWA ambayo imekwenda sambamba na misimamo ya Israel, Barrell amelaani hatua hiyo ya Washington ambayo amesema ni ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema nchi yake itatoa jibu kwa uamuzi huo uliochukuliwa na Marekani kwa kuongeza maradufu msaada wa fedha inaotoa kwa UNRWA.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh al-Maliki amezitaka nchi zingine zichukue hatua kivitendo za kudhamini mahitaji ya kifedha ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi Wapalestina ili kufidia nakisi ya bajeti iliyosababishwa na kukatwa misaada ya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Josep Borrell

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania yametolewa kujibu uamuzi uliotangazwa siku ya Ijumaa iliyopita na serikali ya Washington kwamba haitendelea tena kutoa misaada kwa UNRWA.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wakimbizi wa Palestina UNRWA liliasisiwa mwaka 1949 kwa mujibu wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lengo likiwa ni kuwapatia misaada na kuwaandalia ajira wakimbizi wa Kipalestina. 

Marekani imechukua hatua ya kukata misaada yake ya kifedha kwa UNRWA ili kukwamisha shughuli za taasisi za kimataifa zinazohusika na mgogoro wa Palestina na kuandaa mazingira ya kuifuta moja kwa moja kadhia ya Palestina.../