Wabahrain waandamana kumuunga mkono Sheikh Issa Qassim
-
Maandamano ya Wabahrain
Idadi kubwa ya Waislamu wa Bahrain leo Ijumaa wamefanya maandamano baada ya Swala ya Ijumaa kandokando ya Msikiti wa Imam Jaafar Sadiq (a.s) wakionyesha uungaji mkono na mshikamano wao kwa Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mtajika wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo.
Katika maandamano hayo ambayo yamefanyika katika Ijumaa ya kwanza ya mwezi wa Muharram katika eneo la al Deraz katika mji mkuu wa Bahrai, Manama washiriki walikuwa wamebeba mabango yenye maandishi yanayomuunga mkono mwanazuoni huyo wa ngazi ya juu wa Bahrain. Tarehe 9 Julai mwaka huu Sheikh Issa Qassim alipelekwa London, Uingereza kwa matibabu baada ya askari usalama wa utawala wa Aal Khalifa kuizingira nyumba yake kwa muda wa miaka 2.
Sheikh Issa Qassim ameshiriki majlisi na waombolezaji wa Sayyid Shuhada, Imam Hussein (a.s) katika moja ya vituo vya Kiislamu mjini London.
Katika upande mwingine, askari usalama wa utawala wa Aal Khalifa leo pia kwa wiki ya 13 mtawalia wameendelea kulizingira eneo la al Deraz na nyumba ya Sheikh Issa Qassim na kuwazuia Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Bahrain kusali Swala ya Ijumaa kama ilivyokuwa katika wiki zilizopita.