Msemaji wa Ansarullah: Tutaigeuza Yemen kuwa 'makaburi' ya wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49432-msemaji_wa_ansarullah_tutaigeuza_yemen_kuwa_'makaburi'_ya_wavamizi
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wamesimama kidete na kwa mara nyingine tena wamethibitisha kwamba, Yemen ni 'makaburi' ya wavamizi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 11, 2018 07:55 UTC
  • Msemaji wa Ansarullah: Tutaigeuza Yemen kuwa 'makaburi' ya wavamizi

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wamesimama kidete na kwa mara nyingine tena wamethibitisha kwamba, Yemen ni 'makaburi' ya wavamizi.

Muhammad Abdul-Salaam ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Muungano wa Marekani-Uingereza na Israel ukishirikiana na mamluki wa ndani na wa nje pamoja na magaidi wa Daesh na al-Qaeda, wakipatiwa mabilioni ya dola huku wakipata uungaji mkono wa anga, baharini na nchi kavu wameshindwa kufikia malengo yao.

Amesema kuwa, kusimama kidete wananchi wa Yemen kumewafanya maadui washindwe kufikia malengo yao haramu katika nchi yao huku hujuma yao ya kijeshi ikikaribia mwaka wake wa nne.

Wanapambano wa Ansarullah ya Yemen

Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Yemen imetoa taarifa na kuthamini pamoja na kushukuru misaada ya kibinadamu ya kimataifa kwa wananchi wa nchi hiyo wanaotaabika kutokana na matatizo mbalimbali yakiwemo ya uhaba wa mahitaji muhimu kama chakula.

Taarifa hiyo imetoa wito pia wa kufunguliwa viwanja vya ndege vya Yemen ukiwemo ule wa kimataifa wa Sana'a na kusaidiwa wananchi wa Yemen kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.