Ismail Haniya: Muqawama wa Palestina umevuruga mahesabu yote ya adui Mzayuni
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: Muqawama wa Palestina umevuruga mahesabu ya adui na kubadilisha mlingano wa nguvu.
Ismail Haniya ameeleza kwamba: Kwa ushindi uliopata muqawama, taifa la Palestina limefikia natija na kubainikiwa kwamba, muqawama ndio njia pekee ya kuufikia ukombozi wa Quds na ardhi yote ya Palestina, kwa sababu kuonyesha muqawama kwa muda wa chini ya wiki moja tu kumeleta ushindi dhidi ya utawala ghasibu na kusambaratisha operesheni za kiusalama za utawala wa Kizayuni.
Haniya amesisitiza kuwa, muqawama unaendelea kupanuka na kustawi; na taifa la Palestina linaunga mkono muqawama; na vikosi vya wanamapambano wa muqawama vimetoa jibu kwa utawala wa Kizayuni kulingana na jinai na uchokozi uliofanya.
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ameashiria kujiuzulu Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni, Avigdor Lieberman na kueleza kwamba, kwa kujiuzulu Lieberman umepatikana ushindi mkubwa wa kisiasa; na tangazo lake la kujiuzulu, maana yake hasa ni kutangaza kushindwa utawala huo ghasibu.
Katika upande mwingine, Qudura Faris, mkuu wa klabu ya mateka ya Palestina ameiambia kanali ya televisheni ya Al-Alam kuwa, kwa muda sasa utawala wa Kizayuni umekumbwa na mgogoro; na kujiuzulu Liberman kunaonyesha hali ya mgogoro ulioukumba utawala huo haramu. Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umeshaelewa vyema kwamba hauwezi kupata ufumbuzi kwa njia ya kijeshi na uwezo wake wa kuzuia hujuma uliokuwa ukijigamba na ukijivunia kila mara umesambaratishwa na mashujaa wa muqawama.../