Magaidi Syria wapokea 'drones' 100 za kufanya hujuma za kemikali Idlib
(last modified Tue, 04 Dec 2018 14:43:05 GMT )
Dec 04, 2018 14:43 UTC
  • Magaidi Syria wapokea 'drones' 100 za kufanya hujuma za kemikali Idlib

Kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra la Syria limepokea ndege zisizo na rubani zipatazo 100 litakazozitumia kufanya mashambulizi ya kemikali za sumu katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa nchi.

Shirika la habari la Sputnik la Russia limenukuu duru za kuaminika zikisema kuwa 'drones' hizo zimepelekwa nchini Syria na kukabidhiwa magaidi hao kupitia mji wa Harem, ambao uko katika mpaka wa nchi hiyo na Uturuki.

Inaarifiwa kuwa, magaidi wa Jabhatu Nusra raia wa Morocco na Libya ndio waliopokea ndege hizo zisizo na rubani na kwamba wanapokea mafunzo ya kiufundi kutoka kwa mtaalamu wa Uingereza kuhusu namna ya kuzitumia, na kuzifanya ziwe nyepesi lakini zenye uwezo wa kubeba vichwa vya silaha hizo hatari za kemikali ya sumu.

Haya yanajiri wiki mbili baada ya watu zaidi ya 70 kulazwa hospitalini baada ya magaidi hao wanaoungwa mkono na Marekani kufanya shambulizi la silaha za gesi ya sumu katika mji wa kaskazini mwa Syria wa Aleppo.

Magaidi wa Jabhatu Nusra wanaoungwa mkono na Marekani na nchi za Magharibi

Aidha Novemba 22, shirika hilo la Sputnik liliripoti kuwa, wataalamu wa Ufaransa wanatoa mafunzo na kuwasaidia magaidi mbinu za kutumia silaha za kemikali na jinsi ya kubeba vichwa vya silaha hizo hatari, katika mkoa huo wa Idlib.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma kubwa na ya pande zote ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakisaidiwa na kufadhiliwa na Saudi Arabia, Marekani na washirika wao kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo na kudhamini usalama wa utawala haramu wa Israel.