Timu nyingine ya magaidi wa Daesh yasambaratishwa nchini Iraq
Vikosi vya ulinzi vya Iraq vimetangaza habari ya kusambaratishwa timu nyingine ya magaidi huko magharibi mwa mji wa al Ramadi, makao makuuu ya mkoa wa al Anbar.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AlSumaria News la nchini Iraq, idara ya usalama wa kijeshi ya nchi hiyo imetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, jeshi la Iraq limefanikiwa kusambaratisha timu hiyo ya magaidi saba wa Daesh katika wilaya ya Hiit ya mkoa wa al Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, magaidi hao walikuwa wakifanya shughuli zao kwa siri na walikuwa wanajiandaa kufanya shambulio la kigaidi dhidi ya wananchi wa Iraq.
Katika upande mwingine, askari wa kikosi cha 88 cha jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi leo limetangaza habari ya kuvunja shambulio la magaidi wa ISIS katika eneo la al Muutasim la kusini mashariki mwa Samarrah.
Mwezi Disemba 2017 maeneo yote ya Iraq yaliyokuwa mikononi mwa magaidi wa Daesh yalikombolewa. Hata hivyo wanamgambo wa genge hilo la wakufurishaji wamekuwa wakifanya mashambulizi ya hapa na pale hususan katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi pamoja na kwenye viunga vya mji mkuu Baghdad.
Mara kwa mara vikosi vya ulinzi vya Iraq vimekuwa vikisambaratisha vikundi vya kigaidi vyenye mfungamano na magaidi wa ISIS.