Kamanda wa Jeshi la Israel afanya safari ya siri nchini UAE
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50195-kamanda_wa_jeshi_la_israel_afanya_safari_ya_siri_nchini_uae
Kamada wa Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni amefanya safari ya siri katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2018 23:14 UTC
  • Kamanda wa Jeshi la Israel afanya safari ya siri nchini UAE

Kamada wa Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni amefanya safari ya siri katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi.

Kanali ya Kizayuni ya Makan imefichua kuwa Gadi Eizenkot Mkuu wa Jeshi la Utawala wa Israel mwezi ulioptia wa Novemba alifanya safari ya siri nchini UAE na kukutana na Sheikh Mohammed bin Zayed, Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhab  ambaye pia ni Naibu Kamanda wa Majeshi ya UAE. Aidha katika safari hiyo Eizenkot alikutana na maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la UAE.

Kanali ya Kizayuni ya Makan imemnukulu  Mort Fridman mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Umma wa Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel (AIPAC) akisema kuwa katika mkutano wao huo, mkuu wa majeshi ya utawala wa Kizayuni na mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi, waliafikiana kuwa, Israel itaiuzia UAE silaha; na maafisa wa kijeshi wa UAE watatembelea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Mrithi wa Ufalme wa Saudia Bin Salman yuko mstari wa mbele kujikurubisha na utawala haramu wa Israel

Fridman alifichua hivi karibuni katika mkutano ndani ya sinagogi moja huko New Jersey nchini Marekani kuwa, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu atatembelea Bahrain. Aidha aliongeza kuwa Saudi Arabia ni mshirika wa karibu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika masuala yote ya kieneo na kimataifa.

Saudi Arabia na UAE katika miezi ya hivi karibuni zimekuwa zikipuuza suala la ukombozi wa Palestina na kutotilia maanani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Watawala wa Riyadh na Abu Dhabi wamechukua hatua za pupa na ukurupukaji katika kujikurubisha na kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.