Kufikia tamati majukumu ya Staffan de Mistura katika faili la Syria
(last modified Sat, 22 Dec 2018 02:55:03 GMT )
Dec 22, 2018 02:55 UTC
  • Kufikia tamati majukumu ya Staffan de Mistura katika faili la Syria

Staffan de Mistura, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria ametoa ripoti yake ya mwisho katika Baraza la Usalama na kutangaza rasmi kufikia tamati majukumu yake nchini Syria.

Hadi kufikia sasa Umoja wa Mataifa umekuwa na wawakilishi maalumu watatu katika masuala ya Syria. Mwakilishi wa kwanza maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria ambaye alihesabiwa pia kama mwakilishi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu alikuwa Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa umoja huo. Kofi Annan alishikilia wadhifa huo kwa muda wa miezi sita tu, kuanzia Februari hadi Agosti 2012 na kujiuzulu baada ya kugonga ukuta mpango wa amani wa Syria. Nukta muhimu ni hii kwamba, baada ya Kofi Annan kujiuzulu, wakati alipoulizwa, nani atachukua nafasi yake alijibu kimafumbo kwa kusema: Kuna wapumbavu wengi tu duniani ambao wanaweza kubeba jukumu hili.

Mwakilishi wa pili maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria alikuwa Lakhdar Brahimi mwanadiplomasia kutoka Algeria ambaye alishikilia jukumu hilo kwa muda wa miaka miwili kuanzia 2012 hadi 2014. Katika kipindi chake, mgogoro wa Syria ulishadidi; na kivitendo juhudi zake hazikuzaa matunda yoyote yale ya maana. 

Lakhdar Brahimi alikuwa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria kuanzia mwaka 2012-2014

Staffan de Mistura, mwanadiplomasia Msweden-Mtaliano ni mwakilishi maalumu wa tatu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria ambaye aliteuliwa kuchukua wadhifa huo katika kipindi cha Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Ban Ki-moon. Hivi sasa ambapo Staffan de Mistura anatangaza kuachia ngazi, inapita miaka miwili ya uongozi wa Antonio Guterres kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Staffan de Mistura amekuwa mwakilishi maalumu wa UN katika masuala ya Syria kwa takribani miaka minne na nusu. 

Hata hivyo, kupoa na kupungua mgogoro wa Syria hakujatokana na juhudi zake, bali ni matokeo ya azma na nia thabiti ya jeshi la Syria na washirika wake katika kupambana na ugaidi na kadhalika juhudi za kidiplomasia za Russia, Iran na Uturuki. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, magaidi nchini Syria wamechezea vipigo na kushindwa mtawalia na hivi sasa ni sehemu ndogo tu ya ardhi ya nchi hiyo ambayo iko katika udhibiti wa makundi ya magaidi hao. Wakati huo huo, ubunifu wa kidiplomasia nao ambao unafuatiliwa na Moscow, Tehran na Ankara kwa sehemu kubwa umefungua fundo la mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Staffan de Mistura mwenye umri wa miaka 71, kabla ya kuanza majukumu yake kama mwakilkilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria, katika miaka ya 2001-2004 alikuwa mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, mwaka 2007-2009, mwakilishi maalumu wa UN nchini Iraq na mwaka 2010-2011 alikuwa na wadhifa kama huo, lakini huko nchini Afghanistan. Kwa muktadha huo, hatuwezi kusema kwamba, kushindwa kwake kupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria kunatokana na uanagenzi na kutokuwa na tajiriba na uzoefu wa kutosha.

Sababu kuu ya kushindwa de Mistura, na Umoja wa Mataifa kwa ujumla katika kadhia ya Syria tunaweza kuitoa kwenye tafsiri ya maneno ambayo hayakuwa ya kidiplomasia aliyotamka Kofi Annan, lakini yaliyokuwa yamebeba maana kubwa, kwamba: Kuna wapumbavu wengi duniani ambao wanaweza kubeba jukumu hili.

Inaonekana kuwa, Kofi Annan aling'amua mapema mno kwamba, madola ya kigeni yanayoupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad na ambayo yanayaunga mkono makundi ya kigaidi kwa hali na mali, ndio kizingiti kikuu cha mgogoro wa nchi hiyo. Utendaji wa de Mistura wakati fulani, kikiwemo kipindi cha kufanyika mazungumzo ya Astana kuhusu Syria, ulionyesha kuwa, Umoja wa Mataifa na mwakilishi wake maalumu, badala ya kutopendelea upande wowote katika mgogoro wa Syria, wamekuwa wakisukuma mbele gurudumu la malengo na siasa za madola yanayoupinga utawala wa sasa wa Syria hususan Marekani.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Uturuki na Russia

Hapana shaka kuwa, mwenendo huu ndio sababu kuu ya kufeli Umoja wa Mataifa katika kulishughulikia faili la Syria. Katika uwanja huo, Kanali ya Televisheni ya al-Mayadeen imetangaza katika ripoti yake kwamba:

Katika mkutano wa mwisho wa Geneva uliofanyika wiki hii wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Russia na Uturuki kuhusiana na Syria, Staffan de Mistura hakuwa tayari kuunga mkono tangazo la makubaliano ya nchi tatu hizo na alikuwa na nia ya kuongeza majina matano ya watu wa Marekani katika faharasa ya Kamati ya Kutunga Katiba ya Syria.

Geir O Pedersen mwanadiplomasia wa Kinorway aliyechukua mikoba ya Staffan de Mistura, anatarajiwa kuanza majukumu yake kama mjumbe maalumu wa nne wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria Januari mwakani, katika hali ambayo, kwa upande mmoja kuundwa Kamati ya Kutunga  Katiba ya Syria litakuwa jambo lake la kwanza la kulipa kipaumbele; na kwa upande mwengine, Rais Donald Trump wa Marekani ameshatangaza kuwa, wanajeshi wa nchi yake wataondoka katika nchi hiyo ya Kiarabu.