Vyombo vya habari vya Kizayuni: Msimu wa Machipuo wa Syria umewadia
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimekiri kuwa Syria na rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad wameibuka washindi dhidi ya njama za nchi za Kiarabu na za Magharibi na kutangaza kuwa msimu wa machipuo wa Syria umewadia.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeonyesha kutiwa wasiwasi na mabadiliko ya kasi yanayojiri katika matukio ya Syria ikiwemo kuanzishwa tena uhusiano wa kirafiki kati ya nchi mbalimbali na Damascus na kueleza kwamba hatua hizo sambamba na ushindi wa jeshi la Syria dhidi ya makundi ya kigaidi, ni ushindi wa kidiplomasia na kisiasa kwa serikali ya Bashar al-Assad.
Hezi Simantov, mchambuzi wa masuala ya nchi za Kiarabu katika kanali ya 10 ya televisheni ya Israel amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: Hakuna tena kiongozi yeyote wa Kiarabu anayefikiria kuondolewa madarakani Assad; viongozi wa Israel wanapaswa watafakari kwanza kabla ya kufanya uchambuzi na kuzungumza chochote kuhusu Syria.

Samdari Beri, mchambuzi wa masuala ya nchi za Kiarabu katika gazeti la Yedioth Ahronoth, yeye amesema: Rais Omar al-Bashir wa Sudan ana uhusiano wa karibu sana na Saudi Arabia; na lengo la safari yake nchini Syria lilikuwa ni kuandaa mazingira ya kuanzishwa tena uhusiano kati ya Riyadh na Damascus.
Kuhusiana na mafanikio ya kisiasa na kijeshi iliyopata Syria hivi karibuni, tovuti ya DEBKA imeandika: Bashar al-Assad amepata ushindi mitatu mikubwa katika wiki ya karibuni, ambayo ni kuondoka askari wa Marekani nchini humo, kufunguliwa upya ubalozi wa Imarati mjini Damascus na kuingia vikosi vya jeshi la Assad katika mji wa Manbij.../