Abbas: Palestina haitaruhusu Marekani iiuzie Israel Quds Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50559-abbas_palestina_haitaruhusu_marekani_iiuzie_israel_quds_tukufu
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema Wapalestina katu hawataruhusu Marekani iuuze mji mtukufu wa Quds kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, akisisitiza kuwa mji huo unaokaliwa kwa mabavu ni mji mkuu wa daima wa taifa la Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 01, 2019 08:17 UTC
  • Abbas: Palestina haitaruhusu Marekani iiuzie Israel Quds Tukufu

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema Wapalestina katu hawataruhusu Marekani iuuze mji mtukufu wa Quds kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, akisisitiza kuwa mji huo unaokaliwa kwa mabavu ni mji mkuu wa daima wa taifa la Palestina.

Katika hotuba ya jana Jumatatu kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 54 tangu kuasisiwa harakati ya Fath mjini Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Abba alisema "Quds sio ya kuuzwa".

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amebainisha kuwa, "Hatutamruhusu yeyote ale njama dhidi ya Quds (Jerusalem). Quds itasalia kuwa mji mkuu wa kudumu wa Palestina, kama ambavyo hayati rais Yasser Arafat  alivyosisitiza na kusema kwamba, mtoto wa Kipalestina atapeperusha bendera ya taifa la Palestina katika kuta, minara (ya Misikiti) na Makanisa ya Baitul Muqaddas." 

Hivi karibuni pia, Abbas alisema mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' hautafanikiwa na kwamba, njama zilizoanza tangu kutolewa 'Tangazo la Balfour' mwaka 1917 zingali zinaendelea.

Njama za Trump za kuuyahudisha mji wa Quds

Kwa mujibu wa mpango wa serikali ya Marekani wa 'Muamala wa Karne', mji wa Beitul-Muqaddas utakabidhiwa kwa utawala haramu wa Israel, wakimbizi Wapalestina hawatakuwa tena na haki ya kurejea kwenye ardhi zao za asili na nchi ya Palestina itakuwa sehemu zilizobaki tu za ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo wa kidhalimu, mamlaka ya kusimamia msikiti mtukufu wa al-Aqsa zitakabidhiwa kwa pamoja Jordan, Palestina na utawala haramu wa Israel.