Harakati ya Ansarullah ya Yemen yasisitiza kuheshimu makubaliano ya Stockholm Sweden
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameashiria kuheshimu na kufungamana Harakati ya Ansarullah na makubaliano ya ya Stockholm Sweden na kusema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia unapaswa kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo.
Muhammad Ali al-Houthi amesema hayo leo na kubainisha kwamba, Umoja wa Mataifa nao unapaswa kuushinikiza upande wa pili nchini Yemen ili utekeleze makubaliano hayo ya Stockholm Sweden.
Duru ya nne ya mazungumzo ya amani ya Yemen ilifanyikak Disemba mwaka jana huko Stockholm Sweden kwa kuhudhuriwa na pande husika nchini Yemen pamoja na Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ambapo miongoni mwa yaliyofikiwa katika mkutano huo ni kusitisha vita katika mji na bandari ya al-Hudaydah, kushughulikia hali ya kibinadamu katika mji wa Taiz, kubadilishana mateka na kufunguliwa Uwanja wa Kimataifa wa Sana'a.
Licha ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen na jeshi la nchi hiyo kutekeleza makubaliano hayo, lakini muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umeendelea kukiuka makubaliano hayo.
Umoja wa Mataifa tarehe 29 mwezi Disemba mwaka jana ulithibitisha katika taarifa yake rasmi kwamba, wapiganaji wa Ansarullah pamoja na jeshi la Yemen tayari wameondoka katika mji wa bandari wa al Hudaydah.
Mazungumzo ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen yamekuwa yakigonga mwamba mara kwa mara kutokana na vizingiti vya Saudi Arabia na waitifaki wake.