HAMAS yaionya Israel isiendelee kuushambulia Ukanda wa Ghaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS leo imetoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuonya kuhusu madhara ya uchokozi wake katika Ukanda wa Ghaza.
Fauzi Barhoum, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina amesema kuwa, kuendelea vitendo vya kipuuzi vya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina kama vile kuwashambulia na kuwakandamiza waandamanaji wa Kipalestina wanaopigania haki ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao pamoja na kushambulia vituo vya wanamapambano wa Kipalestina ni chokochoko za hatari sana. Amesema: Uchokozi huo kamwe hauwezi kuwadhaminia usalama na utulivu wanajeshi wa Israel na wala wakazi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Msemaji huyo wa HAMAS pia amesema kuwa, ni jukumu la kitaifa na kimaadili la muqawama wa Palestina kuulazimisha utawala wa Kizayuni utii matakwa ya taifa la Palestina na kwamba stratijia hiyo ya muqawama wa Palestina ndiyo inayoidhamini maslahi na matakwa ya taifa hilo kwa hivi sasa.
Itakumbukwa kuwa ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zimeshambulia maeneo ya wanamuqawama wa Paeltina katika eneo la Hay al Tuffah mashariki mwa Ghaza na pia Khan Yunus, kusini mwa ukanda huo uliozingirwa kidhulma na kila upande na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mizinga ya utawala wa Kizayuni nayo imeshambulia maeneo ya wanamuqawama wa Palestina mashariki mwa Ukanda wa Ghaza.