Iraq yaionya Israel: Msifikirie kabisa kushambulia ardhi yetu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51159-iraq_yaionya_israel_msifikirie_kabisa_kushambulia_ardhi_yetu
Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq ametoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuonya usifikirie kabisa kushambulia ardhi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 28, 2019 02:44 UTC
  • Iraq yaionya Israel: Msifikirie kabisa kushambulia ardhi yetu

Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq ametoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuonya usifikirie kabisa kushambulia ardhi ya nchi hiyo.

Ali Jabbar ametoa onyo hilo katika mahojiano aliyofanyiwa na mtandao wa habari wa "al Ma'aluma" wa Iraq na kusisitiza kuwa: Serikali ya Baghdad itachukua hatua kali za kukabiliana na shambulio lolote la utawala wa Kizayuni iwapo duru za kuaminika za kijeshi zitathibitisha kuwa Israel ina nia ya kushambulia ardhi ya Iraq.

Amesema, Israel haithubutu kufanya shambulio lolote la anga katika ardhi ya Iraq akisisitiza kuwa, hata katika makubaliano ya Baghdad-Washington imesisitizwa kuwa Marekani ina wajibu wa kujibu shambulio lolote la nje hata la Israel dhidi ya Iraq.

Kikosi cha al Hashd al Shaabi cha wananchi wa Iraq

 

Gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post liliandika siku ya Alkhamisi kwamba Iraq imegeuka kuwa shabaha ya mashambulizi ya kijeshi ya Tel Aviv katika kile kinachodaiwa na utawala wa Kizayuni kwamba ni kuizuia Iran kuwa na mawasiliano ya ardhini na nchi mbili za Syria na Lebanon.

Kabla ya hapo pia, Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisema katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi mjini Baghdad kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel una nia ya kushambulia maeneo ya vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo maarufu kwa jina la "al Hashdu al Shaabi."