Feb 17, 2019 04:35 UTC
  • Amnesty International: Idadi ya wakimbizi wa Kisaudia nje ya nchi inaongezeka

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, idadi ya raia wa Saudi Arabia wanaoomba hifadhi na ukimbizi katika nchi mbalimbali duniani inaendelea kuongezeka na kwamba, hiyo ni ishara ya kuporomoka sana uhuru wa kiraia, kijamii na kidini nchini humo.

Msemaji wa Amnesty International amewaambia waandishi habari kwamba, idadi ya Wasaudia wanaoomba hifadhi nje ya nchi iliongezeka mara tatu mwaka 2017 na kwamba kuongezeka kwa Wasaudia wanaoomba hifadhi nje ya nchi na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali ndani ya nchi ni kielelezo cha hali mbaya ya uhuru wa kusema na kujieleza katika nchi hiyo ya kifalme.

Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Takwimu cha Umoja wa Ulaya (Eurostat) zinaonesha kuwa, raia wa Saudi Arabia walioomba hifadhi na ukimbizi nchini Ujerumani peke yake katika miaka minne ya hivi karibuni imefikia 180 na Wasaudia 700 katika nchi zote za Ulaya ikilinganishwa na kipindi cha kati ya mwaka 2011 na 2014 ambapo idadi hiyo ilikuwa Wasaudia 210 tu.

Awali Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilikuwa tayari limetangaza kuwa, idadi ya raia wa Saudi Arabia waliokimbilia nje ya nchi imeongezeka kwa asilimia 317 katika mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka 2012.

Hata hivyo jarida la The Economist la Uingereza limeandika kuwa, tamwimu za idadi ya raia wa Saudi Arabia wanaokimbilia nje ya nchi na kuomba hifadhi ni kubwa zaidi ya hiyo inayotajwa kwa sababu Wasaudia wengi wanaokandamizwa na kuamua kikimbilia nje hawana ujasiri wa kuomba hifadhi rasmi wakichelea maisha yao.

Bin Salman anatuhumiwa kuamuru mauaji ya Jamal Khashoggi nchini Uturuki

Hali ya wanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya kijamii imekuwa mbaya zaidi nchini Saudi Arabia hususan baada ya Muhammad bin Salman kuteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Tags