Hizbullah: Marekani haiwezi kamwe kubadili msimamo wa muqawama
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, misimamo ya Marekani ni misimamo ya kidhalimu, kidikteta na inayokinzana na maslahi ya mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati na hivyo haitaweza kubadili misimamo ya muqawama.
Sheikh Naim Qassem amesema kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani na baadhi ya viongozi wa nchi hiyo daima wamekuwa wakiunga mkono utawala dhalimu wa Israel na kwamba njama za mradi wa Muamala wa Karne ni kutaka kufuta kadhia ya Palestina na Wapalestina. Amezidi kubainisha kwamba sababu kuu na ya msingi ya ya kurefusha vita nchini Syria inatokana na utegemezi wa baadhi ya viongozi wa mirengo ya kisiasa nchini Lebanon na baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kwa Marekani na kuonyesha masikitiko yake kwa mwenendo wa watawala hao wanaotegemea himaya ya Washington kwa ajili ya kulinda vyeo na madaraka yao.
Katika sehemu nyingine Sheikh Ekrima Sa'id Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa na mkuu wa Kamati Kuu ya Kiislamu katika mji wa Quds sambamba na kubainisha kwamba tamaa ya utawala haramu wa Kizayuni kwa msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu haina mwisho, amebainisha kwamba hatua ya kuwakamata wanaharakati wa Kipalestina inayofanywa na utawala huo haiwezi kupunguza irada ya taifa la Palestina kwa ajili ya kufikia malengo yake makuu na badala yake ndio kwanza inazidisha umoja na mshikamano wake. Ameshiaria mafanikio ya Wapalestina ya katika kufungua mlango wa 'Babu al Rahma' moja ya milango ya msikiti wa al-Aqsa baada ya kupita miaka 16 na kufafanua kuwa, moyo wa matumaini ya kuishi kwa amani ya wakazi wa Quds bado unaendelea na kwamba Wapalestina wanaweza kusambaratisha njama chafu za utawala haramu wa Kizayuni. Ijumaa iliyopita mamia ya Wapalestina walielekea kwa wingi upande wa Msikiti wa al-Aqsa katika mlango unaoitwa Babu al Rahma wa kuingilia msikiti huo na kufanikiwa kuufungua, baada ya kufungwa na utawala pandikizi wa Israel kwa miaka 16.