Vijana wawili wa Kipalestina wauawa shahidi kwa kupigwa risasi na Wazayuni
Vijana wawili wadogo wa Kipalestina wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Jeshi la Israel limetangaza kuwa, Wapalestina kadhaa leo wameshambulia gari moja la jeshi hilo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo Wapalestina watatu walilengwa na risasi za wanajeshi hao ambapo wawili kati yao waliuawa huku mmoja akijeruhiwa.
Vijana hao wa Kipalestina wameuawa shahidi masaa machache baada ya mashambulio ya ndege za kijeshi za Israel katika maeneo kadhaa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeendelea kukosoa siasa za Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Hivi karibuni harakati hiyo ilinukuliwa ikisema kuwa, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina anakubaliana na mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" lakini viongozi wa Fat'h wanataka kumuonyesha kiongozi huyo kwamba, anaupinga mpango huo.
Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Mumala wa Karne", mji wa Quds utakabidhiwa kwa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea kwao, utawala haramu wa Israel utasimamia usalama wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vivuko vya mpakani huku maeneo pekee ya Kiarabu ya Quds Mashariki yakiunganishwa na nchi ya Palestina.
Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo eneo la Ukanda wa Gaza litaunganishwa na nchi mpya ya Palestina kwa sharti la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina HAMAS kukubali kuweka chini silaha.