Palestina: Ripoti ya Marekani inadhihirisha uhasama wao kwa Wapalestina
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani vikali hatua ya Marekani ya kudondosha maneno "inayokaliwa kwa mabavu na Israel" kuashiria Miinuko ya Golan, na "maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu" katika ripoti yake mpya haki za binadamu ya kila mwaka.
Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa leo Ijumaa imesema kuwa, kitendo cha Marekani kuondoa maneno hayo kwenye ripoti yake kwa mara nyingine tena kimedhihirisha sera za uhasama za utawala wa (Rais Donald) Trump kwa Wapalestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema ripoti hiyo eti ya haki za binadamu ya kila mwaka iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imepuuza muktadha sahihi wa kisiasa na kisheria kwa kukataa kutumia maneno hayo.
Wapalestina wamekanusha vikali ripoti hiyo, wakisisitiza kuwa lengo la ripoti hiyo ya Marekani ni kupotosha utambulisho wa utaifa wa Wapalestina na historia yao pana ndani ya ardhi zao.
Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuondoa maneno "Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel" kwenye ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatano iliyopita, ilifuta pia maneno haya: "Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi".
Milima ya Golan ilitekwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967. Eneo hilo lina ukubwa wa takriban kilomita mraba 1,200. Utawala wa Kizayuni unadai kuwa ni sehemu ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.