Jihadul Islami yawaonya Wazayuni wasithubutu kushambulia Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52394-jihadul_islami_yawaonya_wazayuni_wasithubutu_kushambulia_ghaza
Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu kufanya shambulio lolote dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2019 09:05 UTC
  • Jihadul Islami yawaonya Wazayuni wasithubutu kushambulia Ghaza

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu kufanya shambulio lolote dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon imemnukuu Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina, Ziad al-Nakhla akisema hayo leo Jumatatu na kutahadharisha kwamba shambulio lolote litakalofanywa na adui Mzayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza litapata majibu makali kutoka kwa muqawama wa Palestina.

Duru za Israel zimetangaza kuwa, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu jana usiku alikatisha safari yake ya mjini Washington Marekani ambako ameonana na rais wa nchi hiyo, Donald Trump. Netanyahu alikuwa amepanga pia kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha lobi ya Kizayuni ya nchini Marekani, AIPAC hata hivyo amekatisha safari yake hiyo na kurejea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, baada ya mji mkuu wa Israel, Tel-Aviv kushambuliwa kwa makombora ya wanamuqawama wa Palestina.

Nembo ya harakati ya Jihadul Islami ya Palestina

 

Mapema leo asubuhi, vyombo vya habari vya kimataifa vimetangaza kuwa, jana usiku kulifanyika shambulizi la makombora lililopiga Tel-Aviv na kujeruhi Wazayuni wasiopungua saba. Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, makombora hayo yamelengwa na wanamuqawama wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza.

Netanyahu amedai kuwa atajibu shambulizi hilo. Jihadul Islami ya Palestina imemuonya kwa kumwambia kuwa shambulio lolote dhidi ya Ukanda wa Ghaza halitopita vivi hivi bila ya kupata majibu makali kutoka kwa wanamuqawama wa Palestina.