Wizara: Israel inatumia gesi za sumu dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Gaza amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia gesi za sumu dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina katika ukanda huo.
Ashraf al-Qidra amesema mbali na wanajeshi wa Israel kutumia risasi hai na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji Wapalestina ambao wamekuwa wakikusanyika katika mpaka wa Ukanda wa Gaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu, lakini askari hao makatili wamekuwa wakitumia pia gesi hatari za sumu dhidi ya waandamanaji hao.
Amesema kemikali za sumu zilizoko kwenye gesi hizo ni hatari kwa afya, ambapo ima humuua muathirika taratibu au kumsababishia ulemavu wa daima.
Waziri wa Afya wa Ukanda wa Gaza amesema wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiwafyatulia Wapalestina mabomu yenye gesi na kemikali hizo hatarishi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, waandamanaji wa Kipalestina 271 wameuawa shahidi huku wengine 16,500 wakijeruhiwa katika hujuma za askari katili wa Israel katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
"Maandamano ya Haki ya Kurejea" yamekuwa yakifanyika kila wiki tokea Machi 30 mwaka jana, ambapo Wapalestina wanautaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao, sambamba na kuruhusiwa wakimbizi wote Wapalestina warejee katika ardhi zao za jadi.