Mashinikizo ya wananchi yawalazimisha Wazayuni kuvunja safari ya kwenda Bahrain
Ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni uliokuwa umepanga kwenda mjini Manama, Bahrain kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa kiuchumi umelazimika kuvunja safari hiyo kutokana na upinzani mkali wa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kumnukuu Jonathan Ortmans, mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama akisema kuwa, ijapokuwa utawala wa Bahrain uliushauri ujumbe huo wa Israel kushiriki katika mkutano huo, lakini leo Jumapili, Wazayuni hao wameamua kutoshiriki mkutano huo wakidai kuwa masuala ya kiusalama ndiyo yaliyowafanya wachukue uamuzi huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua ya ujumbe huo wa Israel ya kuvunja safari yake nchini Bahrain imechukuliwa baada ya bunge la nchi hiyo kulaani kualikwa Wazayuni katika mkutano huo.
Kabla ya hapo duru mbalimbali za nchini Bahrain zilikuwa zimetangaza kuwa Wazayuni 45 wakiongozwa na Eli Cohen, waziri wa uchumi wa utawala wa Kizayuni walipanga kushiriki mkutano wa kimataifa utakaofanyika kuanzia kesho Jumatatu tarehe 15 Aprili 2019 na kuendelea hadi tarehe 18 mwezi huu.
Ukiachana na utawala kibaraka wa ukoo wa Aal Khalifa huko Bahrain, wananchi Waislamu wa nchi hiyo ya Kiarabu wanapinga mno jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hii ni katika hali ambayo wimbi la harakati za mapinduzi na za kupigania utawala wa katiba uliochaguliwa na wananchi lilianza mwezi Februari 2011 nchini Bahrain. Hata hivyo Saudi Arabia ilituma jeshi lake katika kisiwa hicho cha Bahrain na hadi leo hii wanajeshi hao vamizi wanaendelea kukandamiza raia wanaoandamana kwa njia za amani.