Answarullah: Baadhi ya tawala za Kiarabu zinaharakia kufutwa kadhia ya Palestina
Msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen amesema kuwa, baadhi ya tawala za Kiarabu zina pupa ya kutaka kufutwa haraka kadhia ya Palestina, kuliko hata utawala adui wa Kizayuni.
Mohammed Abdul-Salam amesisitiza kwamba Palestina imegeuka kuwa kadhia isiyo na umuhimu wowote kwa tawala nyingi za Kiarabu, lakini akaongeza kwamba, raia wa nchi za Kiarabu kamwe hawatowaacha mkono Wapalestina. Amesema kuwa, uungaji mkono wa tawala ambazo hazina kheri yoyote kwa raia wao na ambazo zinafuata siasa na amri za Marekani, ni jambo lisilofaa hata kidogo.
Msemaji wa Harakati ya Answarullah nchini Yemen ameongeza kwamba, njia ya utatuzi wa kadhia ya Palestina iko mikononi mwa raia wa Palestina ambao wanahitajia kuwa na kiongozi shujaa ambaye atafuata maridhiano ya kitaifa na kuzingatia chaguo la muqawama. Hii ni katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni tawala nyingi za Kiarabu zimekuwa zikijipendekeza kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Marekani sambamba na kuunga mkono mpango muovu wa Washington na Tel Aviv wa Muamala wa Karne.